Yanga yamlilia MO

Muktasari:

Mo alitekwa jana asubuhi akiwa anaelekea kwenye mazoezi katika hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Utani wa jadi si uadui ndicho walichokifanya viongozi wa Yanga umeungana na wenzao wa Simba na Watanzania kwa ujumla kulaani tukio la umeshtushwa na utekwaji wa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’.

Uongozi wa Yanga umesema kitendo hicho kinaleta hofu na kuondoa utulivu katika jamii na kuweka wazi kuwa wapo pamoja naye katika maombi kuhakikisha anarudi salama na kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

MO alitekwa jana alfajiri muda mchache baada ya kushuka katika gari yake tayari kwa ajili ya kuendelea na programu yake ya mazoezi.

Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya alisema wamesikitishwa na utekwaji wa Mo ambaye amesaidia kuleta maendeleo ya soka nchini, hasa kwa watani wao wa jadi Simba, kutoa pole kwa familia yake pamoja na ndugu na jamaa zake wa karibu katika kipindi hiki kigumu wanachokipitia.

“Sijisikii vizuri, nimeamka na kukutana na suala hili la kusikitisha, nawaomba mashabiki na wanachama wa Yanga kuungana na watani zetu ili Mo apatikane salama na kuungana na familia yake na ya michezo kwa ujumla,”.

“Utani wetu ni katika masuala ya michezo, hili tunatakiwa kuwa wamoja kwa kumuombea ili arudishwe salama na kuendelea na majukumu ya kazi zake kama ilivyozoeleka sitaki kuongea sana kwasababu suala hili ndio kwanza linafuatiliwa na polisi,” alisema Kaya.

“Tupo pamoja na wahusika wote tukimuombea kuhakikisha anapatikana akiwa salama na hatua kali za kisheria zifuate mkondo kwa watakaohusika katika utekwaji wa mfanyabiashara na mwanamichezo mwenzetu,” alisema Kaya.

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara aliyefika eneo hilo alisema Simba imeshtushwa na taarifa hiyo na kwamba wanaziachia mamlaka kutafuta alipo MO.

Manara alisema tukio hilo limetokea siku moja baada ya MO kusimamia kikao cha Bodi ya Simba kilichofanyika juzi. Alisema MO wakati wote wa kikao hicho alionekama mchangamfu na mwenye furaha. Jambo hilo limewashtua wajumbe wenzake. “Simba tumeshtushwa sana na tukio hili limetupa kiza kizito tusijue kipi kimemkumba mwenzetu,” alisema Mmanara akiwa katika uso wa huzuni.

“Mo tulikuwa naye jana (juzi) katika kikao cha bodi aliendesha kikao vizuri alikuwa mwenye furaha kama siku zote na kikao kilimalizika salama.”

Zinapokuja taarifa kama hizi zinasumbua lakini wanasimba wenzangu tuwe watulivu tumuombee mwenzetu huko aliko asipatwe na baya lolote, lakini pia tuwaachie jeshi la polisi na serikali kwa ujumla wenye mamlaka ya kulipatia ufumbuzi suala hili,” alisema.