Yanga yalipa kisasi Simba

Muktasari:

Yatibua dili la mido wa AS Vita, Niyonzima na Kotei wafutwa rasmi

MASHABIKI wa Simba walichekelea sana waliposikia mabosi wao wamemvuta winga matata Charles Ilanfya aliyekuwa akiwinda na Yanga tangu msimu uliopita, lakini sasa ni zamu yao ya kununa baada ya matajiri wa Jangwani nao kuamua kuwatibulia Msimbazi dili lao kwa kumbeba mido mmoja matata.

Kiungo huyo ambaye Simba ilishafanya mazungumzo naye na kuelezwa alikuwa anasubiri simu tu na mkataba kutoka Msimbazi, anakipiga klabu ya AS Vita ya DR Congo, lakini kwa sasa amebadilisha mawazo baada ya matajiri wa Jangwani wakiongozwa na Kampuni ya GSM kumalizana naye kibabe.

Ipo hivi. Yanga imebakiza kumtambulisha tu kiungo mkabaji Mukoko Tonombe baada ya kila kitu juu ya dili baina yao kukamilika na sasa jamaa anakuja kucheza pamoja na Mkongo mwenzake Papy Tshishimbi msimu ujao katika kikosi cha Jangwani.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, katika ripoti yao ya usajili ya kocha Luc Eymael ilihitaji kutafutiwa kiungo mkabaji bora na Mukoko akakubalika na sasa msimu ujao ni uhakika atacheza baada ya Mwanaspoti kupenyezewa kila kitu na mabosi wa AS Vita inayomliki kiungo huyo fundi wa mpira.

Taarifa kutoka DR Congo zilizotolewa na Meneja wa AS Vita, Diba Ilunga ni kwamba Yanga kupitia matajiri wa GSM wamemaliza biashara ya kumsajili Mukoko huku akificha gharama za kuvunja mkataba wa kiungo huyo mkabaji.

“Yanga wamemchukua Mukoko. Kilichobaki tu ni mchezaji kuja huko Tanzania. Kila kitu kimekamilika baada ya siku chache atakuja Tanzania, hakuna maneno kabisa ni kiungo mzuri sana,” alithibitisha Ilunga.

Mukoko amekuwa kiungo bora mkabaji wa Vita ambapo ubora wake umechangiwa na kumudu kucheza kama kiungo mkabaji na hata beki wa kati endapo atahitajika kufanya hivyo.

Mapema Kocha Msaidizi wa klabu hiyo ya AS Vita, Raoul Shungu aliliambia Mwanaspoti, hadi mwezi uliopita Mukoko alimwambia kuwa yupo katika mazungumzo na bosi mmoja wa Simba na kwamba alijua anatua kwa Wekundu hao.

“Nimeshangaa sana nilikuwa na Mukoko mwezi uliopita wakati tunaanza mazoezi akaniuliza kuhusu Tanzania ikoje, akanieleza kuwa kuna timu inaitwa Simba inamtaka anaongea nao akataka nimwambie kwa kuwa nimefanya kazi huko,” alisema Shungu aliyewahi kuinoa Yanga na kuongeza;

“Yanga kumchukua Mukoko hapo timu yangu imenifurahisha sana huyu ni kiungo bora sana, inaonekana sasa kuna watu wanafanya usajili kwa umakini sana hapo, wamepata kiungo ambaye atawapa tabu Simba kama bado katika kiungo chao kipo kama kile tulichokutana nacho wakati ule.

KOTEI, NIYONZIMA NDO BASI

Akili ya Yanga kuzuia usajili wa kiungo Mghana James Kotei inaonekana kukaa sawa ambapo usajili huo wa Mukoko utafuta rasmi mbio za kumchukua nyota huyo wa zamani wa Simba sambamba na Mnyarwanda Ally Niyonzima waliyekuwa wakimpigia hesabu hapo awali.

Mpaka sasa Mwanaspoti linafahamu kwamba Yanga itakuwa imechukua mastaa wawili wakubwa kutoka AS Vita ambapo mapema GSM ambao ndio wanafanya usajili katika kikosi cha Yanga ilishamchukua winga Tuisila Kisinda ambaye kila kitu kimeshakamilika akisaini mkataba wa awali wa miaka miwili.