Yanga yakwepa vigogo, yatupwa kwa vibonde Kombe la Shirikisho

Muktasari:

Timu 16 zilizoondolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakutanishwa na timu 16 zilizofuzu hatua ya mwisho ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika kupata idadi ya timu 16 ambazo zitafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Dar es Salaam.Wakati droo ya hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kuchezeshwa leo saa 2.00 usiku jijini Cairo, Misri, presha inaweza isiwe kubwa kwa wawakilishi wa Tanzania, Yanga kutokana na kuepuka kupangwa na vigogo Enugu Rangers (Nigeria), Hassania Agadir, RS Berkane (Morocco),  Zanaco (Zambia), Djoliba (Mali) pamoja El Masry (Misri).

Kwa mujibu wa CAF, Yanga imepangwa Chungu A hivyo itacheza na moja ya timu kutoka Chungu D ambazo nyingi siyo timu tishio katika mashindano ya klabu barani Afrika.

Yanga inaweza kupangwa na moja ya timu 10 kutoka Chungu D lenye timu za DC Motema Pembe (DR Congo), Bandari FC (Kenya), Triangle United (Zimbabwe), Bidvest Wits na TS Galaxy (Afrika Kusini), ESAE FC (Benin) , FC San Pedro (Ivory Coast), Paradou (Algeria), Pyramids FC (Misri) na Proline (Uganda).

Kitendo cha Yanga kupangwa katika chungu A katika upangaji wa droo hiyo leo, kinaifanya ikwepe kukutana na timu sita (6) ambazo zinaonekana ni tishio katika Kombe la Shirikisho kutokana na historia ya kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika, uzoefu wa mechi za kimataifa pamoja na uwekezaji ambao zimefanya.

Kwa mujibu wa utaratibu wa uchezeshaji droo hiyo ambao umetengangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Yanga itapangwa kwenye chungu cha kwanza (chungu A) ambacho kitakuwa na kundi la timu tisa (9) zilizotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo nyingine ni Asante Kotoko (Ghana), Enyimba (Nigeria), Gor Mahia (Kenya), UD Songo (Msumbiji), Horoya (Guinea), KCCA (Uganda) na mshindi wa mechi baina ya Zamalek ya Misri na Generation Foot ya Senegal.

Timu hizo za Chungu A zitakutana na timu 10 za chungu cha mwisho (Chungu D) ambazo ni DC Motema Pembe (DR Congo), Bandari FC (Kenya), Triangle United (Zimbabwe), Bidvest Wits na TS Galaxy (Afrika Kusini), ESAE FC (Benin) , FC San Pedro (Ivory Coast), Paradou (Algeria), Pyramids FC (Misri) na Proline (Uganda).

Katika kundi hilo la timu 10 ni timu tatu tu ambazo zinaonekana kuwa tishio kwa Yanga ambazo ni DC Motema Pembe, Paradou na Pyramids FC

DC Motema Pembe ya DR Congo, kubwa inalojivunia mbele ya Yanga ni uzoefu na mafanikio makubwa ambayo imewahi kuyapata kwenye mashindano ya klabu Afrika, ikiwahi kutwaa Kombe la Washindi Afrika mwaka 1994.

Kwa upande wa Pyramids FC na Paradou ingawa hazina historia kubwa kwenye mashindano ya Afrika, uwekezaji ambao zimefanya kwenye vikosi vyao na kasi ambayo zimekuwa nayo msimu huu kwenye mashindano ya klabu Afrika vinaweza kuwa changamoto kwa Yanga.

Thamani ya kikosi cha Paradou kwa mujibu wa mtandao wa www.transfermarkt.com ni Euro 6 milioni (zaidi ya Shilingi 15 bilioni) wakati kile cha Pyramids FC ya Misri ni kiasi cha Euro 20 milioni (Shilingi 50 bilioni).

Timu nyingine saba katika chungu cha mwisho ambazo mojawapo inaweza kukutana na Yanga, hazijafanya uwekezaji mkubwa lakini pia hazina rekodi wala uzoefu wa kutosha kwenye mashindano ya klabu Afrika kulinganisha na Yanga ambayo ndani ya miaka mine imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili.

Presha huenda ingekuwa kubwa kwa Yanga ikiwa ingepangwa kwenye Chungu C ambacho timu zake zitakutanishwa na zile za Chungu B ambazo zinaonekana kuwa moto wa kuotea mbali ambazo ni Enugu Rangers (Nigeria), Hassania Agadir na RS Berkane (Morocco),  Zanaco (Zambia), Djoliba (Mali) na El Masry (Misri).