Yanga yajichimbia Morogoro kuiwinda Simba

Monday February 11 2019

 

By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam. Homa ya pambano la watani wa jadi Yanga dhidi ya Simba imezidi kupamba moto baada ya Yanga kuamua kujichimbia mapema mkoani Morogoro kwaajili ya mchezo huo.

Klabu hiyo baada ya kucheza michezo yake mitatu mkoani, miwili Tanga na mmoja Singida uongozi wa Yanga uliamua kupitiliza moja kwa moja Morogoro kwenda kuweka kambi.

Hii imekuwa ni kawaida kwa klabu ya Yanga kujichimbia Morogoro hata alipofika kocha Mwinyi Zahera, huku mwenzake wa Simba, Patrick Aussems yeye alishakataa wachezaji wake kushughulishwa kwa kuhamishwa hamishwa.

Wakati huohuo; Simba wiki hii ni ngumu kwao. Kwani kesho watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Al Ahly kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao wanahitaji pointi na magoli mengi ili kujiweka katika sehemu nzuri.

Bado haijafahamika rasmi kama Aussems anaweza akabadilisha uamuzi ya kutoka jijini Dar es Salaam na kwenda Zanzibar au Morogoro, kwani katika mchezo wa raundi ya kwanza aligoma kukitoa kikosi chake Dar.

Yanga na Simba zitashuka uwanjani Jumamosi, huku mchezo huo ukisubiliwa kwa hamu kwa mashabiki wote, baada ya mchezo wa kwanza kutoka sare 0-0.

Advertisement