Yanga yaitibulia Jamhuri

Muktasari:

Bao hilo la Jamhuri lilikuwa kama lililochokoza nyuki kwa Yanga, kwani vijana wa Noel Mwandila walicharuka na kusawazisha kupitia kwa Faraji Kilaza dakika ya 20 akipokea pasi murua ya Pius Buswita.

UNGUJA.UKISIKIA roho mbaya ndio hii. Yanga licha ya kuwa imeshaanga michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019, lakini jioni ya jana iliamua kuwafanyia roho mbaya tu Jamhuri baada ya kuwafumua mabao 3-1 na kuwatibulia wapinzani wao hao kutinga nusu fainali.

Yanga iliyopeleka kikosi cha pili, ilipata ushindi huo katika mechi ya kukamilisha ratiba iliyopigwa Uwanja wa Amaan na kuwakwamisha Jamhuri kuzifuata Simba na KMKM zilizopo Kundi A na Azam na Malindi zilizopenya hatua hiyo kutoka Kundi B.

Katika mchezo huo, Jamhuri iliyokuwa ikihitaji ushindi ili kufufua nafasi ya kupata nafasi moja ya kucheza nusu fainali zitakazochezwa kesho Ijumaa, ndio iliyokuwa ya kwanza kutikisia nyavu za Yanga kupitia Haji Ramadhan katika dakika ya tatu.

Mfungaji alifunga bao hilo kutokana na uzembe wa kipa wa Yanga, Ibrahim Hamid ambaye katika michuano hiyo ameonekana kukosa umakini na kuigharimu timu yake ikiwa ndio kwanza amesajiliwa katika dirisha dogo lililofungwa mwezi Desemba, mwaka jana.

Bao hilo la Jamhuri lilikuwa kama lililochokoza nyuki kwa Yanga, kwani vijana wa Noel Mwandila walicharuka na kusawazisha kupitia kwa Faraji Kilaza dakika ya 20 akipokea pasi murua ya Pius Buswita.

Dakika nane baadaye, Shaaban Mohammed aliandika bao la pili la Yanga baada ya kipa wa Jamhuri kutema shuti la Buswita na yeye kumalizia nyavuni kiulaini, hilo likiwa bao lake la pili kwenye michuano hiyo akila sahani moja na Meddie Kagere wa Simba.

Buswita aliyecheza vizuri kwenye mchezo wa jana aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 32 kwa shuti kali lililoipeleka timu yake mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1 yaliyodumu hadi dakika 90, licha ya mabadiliko kadhaa yaliyofanywa na timu zote.