Yanga yaikimbia Simba Kombe la Kagame

Muktasari:

  • Uamuzi huo wa Yanga unakumbusha historia ya mwaka 2008 ambapo Yanga ikiwa katika hali tete ya kiuchumi ilishindwa kutokea uwanjani kucheza na Simba katika mashindano ya Kombe la Kagame.

Dar es Salaam.  Miaka 10, imepita Yanga imerudia tena kujiondoa katika mashindano ya Kombe la Cecafa kutokana na sababu mashindano hayo yameingiliana na mapumziko ya wachezaji.


Uamuzi huo wa Yanga unakumbusha historia ya mwaka 2008 ambapo Yanga ikiwa katika hali tete ya kiuchumi ilishindwa kutokea uwanjani kucheza na Simba katika mashindano ya Kombe la Kagame.


Yanga ikiwa chini ya aliyekuwa Mwenyekiti Imani Madega iligomea mchezo huo kwa madai ilipwe Sh50 milioni kabla ya kupeleka timu uwanjani.


Simba iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Hassani Dalali ilikuwa kwenye kiwango bora licha ya kutolewa katika hatua ya nusu fainali kwenye mashindano hayo.


Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), iliifungia Yanga miaka mitatu kushiriki mashindano hayo na kulipa faini Dola 35,000.


 Mapema leo Uongozi wa klabu ya Yanga umethibitisha kutokushiriki mashindano ya Kombe la Kagame.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwingi Zahera alisema ratiba ya mashindano hayo yameingia ratiba yao hivyo hawatoweza kushiriki kutokana na mazingira yao.


Alisema Yanga haina kikosi kipana wachezaji wengi walio na uzoefu ni majeruhi wamekuwa wakitumia vijana ambao wamekuwa na matokea mabaya hivyo hawana sababu ya kushiriki na kupoteza jambo ambalo linaharibu taswira ya klabu.


"Tulishatoa taarifa muda mrefu kwamba hatutashiriki, lakini nashangaa kuona timu imewekwa katika makundi sasa ni muda wa wachezaji kufanya mapumziko kutokana na kuchoshwa na mashindano mengi mfululizo wakirudi wanaendelea na maandalizi kwaajili ya mashindano ya kimataifa na ligi ya ndani," alisema Zahera.


Uamuzi huo unalengo la kutoa mwanya kwa wachezaji hao kujiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hasa mchezo wao dhidi ya Gor Mahia utakaopigwa Julai 17.


Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 Jijini Dar es Salaam, lakini Simba na Yanga zimepangwa Kundi C. Nyingine ni St George ya Ethiopia na Dakadaha ya Somalia.


Timu hizo zinatarajiwa kukutana uso kwa uso katika mchezo uliiopangwa kupigwa Julai 5 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es  Salaam.


Hata hivyo, Yanga ilitumikia adhabu hiyo kwa mwaka mmoja kabla ya kufunguliwa  kuendelea kushiriki mashindano hayo.