VIDEO: Yanga yafyeka 14, Morrison bado yupo yupo sana

UONGOZI wa Yanga umetangaza nyota 14 waliowaacha huku mchezaji wao wa kigeni Bernard Morrison ataendelea kuitumikia klabu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ingawa bado kuna sintofahamu juu ya mkataba wake.

Wakati Morrison akibaki, nahodha wao Papy Tshishimbi, Mohamed Issa 'Banka', Mrisho Ngassa, David Molinga, Jaffary Mohammed, Tariq Seif, Andrew Vincent wao mikataba yao imemalizika hivyo wameachwa huru.

Hivi karibuni mchezaji huyo raia wa Ghana amekuwa katika msuguano na viongozi wake akidai kwamba hajasaini mkataba mpya huku viongozi wa Yanga wakisema alisaini mkataba mpya ambapo mkataba wa awali wa miezi sita ulimalizika.

Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema Morrison bado wana mkataba nae.
"Morrison ni mchezaji wetu na ndio maana tukasema aende sehemu yoyote kusaini kama kweli anasema hana mkataba," alisema Bumbuli.

Bumbuli amesema wachezaji Ali Mtoni, Ali Ali, Yikpe Gislain, Eric Kabamba, Rafael Daudi, Issa Maundu na Patrick Sibomana hawa wapo katika mazungumzo ya kusitishiwa mikataba ambao wamepeana muda wa wiki moja kuzungumza.

Wachezaji waliobaki kuitumikia Yanga ni Farouk Shikhalo, Ramadhani Kabwili, Metacha Mnata, Haruna Niyonzima, Lamine Moro, Morrison, Faisal Salum, Deus Kaseka, Ditram Nchimbi, Balama Mapinduzi, Abdulaziz Makame, Paul Godrey, Adeyun Saleh, Said Juma Makapu.

Bumbuli amesema kuwa wakongwe Juma Abdul na Kelvin Yondani ambao mikataba yao imemalizika wanaendelea kuzungumza nao kwa ajili ya mikataba mipya.