Yanga ya Kaze ndo inakuja hivyo

KOCHA wa Yanga, Cedrick Kaze amefungua ukurasa wa maisha mapya ya ukocha ndani ya klabu hiyo kwa ushindi katika mechi yake ya kwanza akikiongoza kikosi hicho huku kila mchezaji wake aliyepata nafasi ya kucheza akionyesha uwezo.

Ukiachana na matokeo hayo ambayo Yanga waliyapata ya mshindi wa bao 1-0, dhidi ya Polisi Tanzania habari nyingine ilikuwa ni mfungaji wa bao kiungo Mukoko Tonombe.

Tonombe aliifungia Yanga bao la pili msimu huu na yote yakiamua matokeo ya mechi kwani mara ya kwanza akifanya hivyo ugenini dhidi ya Kagera Sugar waliposhinda bao 1-0.

Kwa namna mchezo wa juzi ulivyokuwa, ni wazi kuwa, kama Kaze atapata muda mrefu wa kukinoa kikosi hicho, vijana hao wa Jangwani watatisha, kwani kuna mambo kadhaa yalibadilika kikosini.

Yanga walicheza soka la kuvutia wakianzia nyuma tofauti na ilivyokuwa chini ya kocha aliyetimuliwa Zlatko Krmpotic, lakini hata Polisi walionyesha walikuja jijini Dar es Salaam kikazi na wangeweza kulazimisha japo sare, kama sio kujichanganya kwa mmoja wa wachezaji wakati akiokoa shuti la Mukoko na kuusindikiza mpira wavuni.

Kama Polisi wangekuwa watulivu, walikuwa na uwezo wa kuendeleza rekodi ya kuigomea Yanga, kwani vijana wao waliupiga mwingi licha ya kukumbana na uzoefu wa nyota wa Jangwani na kuwafanya wapoteze kwa mara ya kwanza mbele ya Yanga tangu wapande msimu uliopita.

Mwanaspoti inakuletea kila ambacho alionyesha mchezaji kwenye mechi hiyo ya Yanga na Polisi.