Yanga wawaombea dua njema Simba

WAKATI presha ya mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba ikizidi kupanda kwa wadau wa timu hizo mbili, Yanga wameamua kuwaombea dua njema watani zao wenye wachezaji majeruhi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ameeleza ni namna gani timu yake inawaombea mema watani wao Simba.

“Tumesikia kuwa ndugu zetu Simba nusu ya wazee (wachezaji) wao wa kikosi cha kwanza ni majeruhi, tunawapa pole sana na tunawaombea dua njema wapone haraka iwezekanavyo wawepo  kwenye mchezo wetu ili tukiwafunga wasipate visingizio,” amesema Bumbuli.

Kuhusu maandalizi ya timu kwa ujumla Bumbuli amesema kila kitu kipo tayari na timu itasafiri kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam kwa ndege baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa leo dhidi ya Gwambina FC.

“Vijana wetu wapo tayari kwa mechi hiyo na kwa sasa wapo huko kanda ya ziwa kwa mechi nyingine za Ligi Kuu ambazo kwetu ni kama mazoezi kuelekea mchezo dhidi ya SImba jumamosi hii, ambapo wanatarajiwa kutua Dar es Salaam muda wowote baada ya mchezo wa leo,” alisema Bumbuli.

Yanga ndio watakuwa wenyeji wa mchezo huo unaotarajiwa kupigwa Novemba 7 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa majira ya saa 11 jioni.