Yanga wapata zali

TAFSIRI ya wachambuzi wa soka ni kwamba, Yanga imepata zali la aina yake kabla ya kuikabili Simba Oktoba 18, kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Itakuwa mechi mbili mfululizo kwenye mkeka huo kabla ya kuwakabili watani wao wa jadi Simba ambao watakuwa wanatokea kwenye viwanja chakavu mikoani.

Mechi mbili za Yanga zitakazopigwa Uwanja wa Mkapa ni dhidi ya Coastal Union (Oktoba 3) na Polisi Tanzania (Oktoba 11), wakati watani wao wa jadi Simba wataifuata JKT Tanzania, mkoani Dodoma mchezo utakaopigwa (Oktoba 4, Uwanja wa Jamhuri) na mchezo wa pili watakwenda Rukwa kucheza na Tanzania Prisons (Uwanja wa Nelson Mandale, Oktoba 10).

Kutokana na presha ya mechi ya watani wa jadi itakayopigwa Oktoba 18, wachezaji wa zamani wameona Yanga itakuwa na faida kujipanga upya kiuchezaji kwani bado hawachezi soka la kuvutia mpaka sasa.

Beki wa zamani wa Simba, Godwin Aswile alisema faida itakayoipata Yanga kucheza mechi mbili mfululizo kabla ya mchezo wa watani wa jadi Oktoba 18 ni kuzoea Uwanja wa Mkapa na hali ya hewa.

“Pamoja na faida watakayoipata Yanga ukweli utabakia palepale kwamba tayari Simba ina kikosi kilichokuwa na muunganiko, tofauti na Yanga ambao kocha bado hajapata kikosi cha kwanza, hivyo bado mechi yao itakuwa ngumu, lakini kitendo cha wao kucheza sana Dar kitawajenga,” alisema.

Naye straika wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila alisema anaona Yanga itafaidika kupata muda wa wachezaji kupumzika, kuzoea uwanja mpaka waje kucheza na Simba anaamini itakuwa kwenye kiwango cha kuwapa matokeo na mchezo wa kuvutia zaidi ya inavyoonekana sasa.

“Mechi za mikoani zina changamoto kwanza inaanzia kwenye viwanja, kama Yanga imeshinda dhidi ya Mtibwa Sugar, haitakubali kupoteza Uwanja wa Mkapa dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania. Na hadi kukutana na Simba itakuwa kwenye kiwango cha hali ya juu kinachoweza kuwapa matokeo,” alisema Lunyamila na kuongeza:

“Tofauti na Simba ikipoteza mchezo mmojawapo mkoani, morali yao itapungua na itakutana na Yanga ikiwa kwenye kiwango kikubwa hivyo inaweza ikawafanya wakapoteza siku hiyo,” alisema.

Ally Mayay alisema faida kwa Yanga kucheza mechi mbili kabla ya kukutana na Simba Uwanja wa Mkapa, faidi ni mbili wachezaji kuzoea mazingira na hali ya hewa, tofauti na Simba itakayotoka kucheza maeneo ya baridi.

“Ingawa sio asilimia 100 Yanga kufaidika na hilo kwasababu Simba nayo inatumia Uwanja wa Mkapa kama nyumbani hivyo hakutakuwa na geni zaidi kwao japokuwa changamoto itakuwa kwenye hali ya hewa,” alisema Mayay na kuongeza:

“Bado Simba itakuwa na muda wa kujipanga kama mechi itachezwa tarehe 10 na ikafika Dar es Salaam tarehe 11, itakuwa na muda mzuri wa kujiandaa kwani katika uwezo sina wasiwasi nao, inacheza kwa mifumo ile ile ambayo inawafanya watengeneze nafasi na wanafunga,” alisema.

Yanga itakutana na Simba inayocheza kitimu na pia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja hivyo eneo la kiungo anaona litakuwa na ushindani zaidi.

SAPRAIZI YA CARLINHOS

Kocha msaidizi, Juma Mwambusi amefichua kwamba kuna sapraizi kibao zinakuja kwa staa huyo.