Yanga walibugi hapa, Azam walikuwa watamu

Muktasari:

Katika mechi na Azam, kikosi cha Yanga kilifanya mambo kadhaa ambayo yalisababisha washindwe kupata ushindi wakati huohuo wapinzani wao wakitumia fursa hiyo kupata ushindi. Mwanaspoti ambalo lilifuatilia mchezo huo liligundua mambo hayo ambayo Yanga na kusababisha kupoteza alama tatu dhidi ya Azam FC.

MWANZO si mzuri kwa kocha mpya wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymeal baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar na Azam Fc, huku akiwa na kibarua kingine kesho Jumatano watakapocheza na Singida United ugenini.

Katika mechi na Azam, kikosi cha Yanga kilifanya mambo kadhaa ambayo yalisababisha washindwe kupata ushindi wakati huohuo wapinzani wao wakitumia fursa hiyo kupata ushindi. Mwanaspoti ambalo lilifuatilia mchezo huo liligundua mambo hayo ambayo Yanga na kusababisha kupoteza alama tatu dhidi ya Azam FC.

MASTRAIKA BADO

Kikosi cha Yanga kwenye mechi na Azam kilianza na straika mmoja - David Ndama ‘Molinga’ ambaye alionekana kuwa bora hasa kipindi cha kwanza akisumbua ngome ya Azam iliyokuwa chini ya mabeki wa kati Daniel Amoah na kinda Oscar Masai.

Molinga aliwasumbua mabeki hao, lakini alionekana kukosa msaada wa mshambuliaji wa pili ambaye alikuwa akicheza Mapinduzi Balama, Haruna Niyonzima pamoja na Kabamba Tshishimbi.

Baada ya kuonekana katika eneo hilo kuna shida na mabeki wa Azam kuwa bora, kocha wa Yanga, Eymael aliwaingiza washambuliajii Ditram Nchimbi na Yikpe Gnamein ambao walitimiza idadi ya mastraika watatu asilia ambao wote kwa pamoja walishindwa kuwa bora mbele ya safu ya ulinzi ya Azam.

WAPYA

Yanga ilianza na wachezaji wapya saba wote wapya waliosajiliwa katika dirisha kubwa na dogo ambao ni kipa Farouk Shikalo, Lamine Moro, Ally Mtoni, Haruna Niyonzima, Mapinduzi Balama, Molinga na Patrick Sibomana.

Kipindi cha pili waliwaingiza Nchimbi na Yikpe na kutimiza wachezaji tisa waliocheza kwenye mechi hiyo wakiwa wapya.

YANGA BILA MPIRA

Wachezaji wa Yanga walionekana kuwa bora pale timu yao ilipokuwa na mpira, lakini walipokuwa hawana walikuwa na makosa mengi - baadhi yao mara chache walikuwa wakijihusisha na shughuli ya kukaba kama Niyonzima na Molinga.

Jambo hilo, kutokuwa makini na kufanya makosa mengi wanapokuwa hawana mpira Azam waliweza kupenya na kuingia kwa urahisi katika eneo la Yanga, ila walikosa umakini wa kutengeneza nafasi za kufunga na kama Yanga wange-cheza na timu ambayo ina uwezo wa kupiga presha pindi wanapokuwa hawana mpira huenda wangepoteza kwa idadi kubwa ya mabao.

Azam walionekana kumiliki mpira muda mwingi katika maeneo mengi kwani wachezaji wa Yanga walishindwa kuwa makini kukaba.

EYMAEL ANA KAZI

Kocha wa Yanga, Eymael bado ana kazi kubwa ya kuifanya kuwa na kikosi bora hasa katika kucheza kwa kuelewana kwani kuna maeneo mengi wameonekana kuwa na shida kama katika safu ya ushambuliaji, kiungo na hata ulinzi ambapo hufanya makosa mengi mara kwa mara. Eymael anatakiwa kutenga muda wa kutosha katika mazoezi ya Yanga na kufanyia kazi upungufu kama timu inapokuwa haina mpira wachezaji wafanye jambo gani kulingana na wapinzani walivyo hivyo hivyo hata wanapokuwa na mpira wanatakiwa kushambulia kwa aina gani.

NIYONZIMA, TSHISHIMBI

Kabla ya Yanga kumsajili kiungo, Niyonzima katika dirisha dogo walionekana kutokuwa na kiungo mshambuliaji mbunifu wa aina yake.

Niyonzima ambaye amebeba matumaini makubwa ya wapenzi wa Yanga katika eneo kiungo ameonyesha umahiri wa kumiliki mpira na kupiga pasi nyingi ambazo huenda hazina faida kwa kuwa zinakwenda pembeni, lakini wakati huohuo unaweza kukuta timu inashambulia kwa haraka akipewa mpira anageuka nyuma.

Hivyo vyote ndivyo alivyofanya katika mechi ya Azam ambayo viungo wa timu pinzani Salum Abobukar ‘Sure Boy’ na Brayson Raphael waliwapa mwanya wa kutawala katika eneo hilo muda wote kwani walipokuwa na mpira walifikiria zaidi kwenda mbele na si kupiga pasi za pembeni au nyuma.

AZAM MBINU

Katika mchezo huo Azam walionekana kuingia na mbinu ya kutaka kumiliki mpira kwa muda mrefu, kushambulia kwa taratibu huku wakipiga pasi fupifupi ambazo ziliwafanya kufika langoni mwa Yanga mara chache, lakini hata mashambuliazi yao hayakuwa ya kutisha sana.

Mbinu hiyo ya Azam iliwanufaisha baada ya kuapata bao la kuongoza dakika 26 kutokana wachezaji wa Yanga wengi wao kutokuwa mahiri katika kukaba na mpira uliendelea kumilikiwa na Azam muda mrefu wakati huohuo wao walipopata walicheza mipira mirefu kwa Molinga, Nchimbi na Yikpe ambayo yote haikuwasaidia.

CIOABA KUWAIGA KAGERA

Mwanaspoti liliona kuwa kocha wa Azam, Aristica Cioaba hakuwa na kazi kubwa kwani ni wazi alionekana kuifuatilia mechi ya Yanga wakipoteza nyumbani kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar siku ya Jumatano wiki iliyopita.

Cioaba alichukua mbinu za Kagera Sugar kumiliki mpira kwa muda mwingi, kupasiana pasi fupifupi, kucheza kwa nidhamu, kuwaheshimu wapinzani na kuzuia mipira ya kushambulia kwa Yanga ambayo huitumia pembeni kwa mabeki na mawinga kushoto na kulia.

CHIRWA, NGOMA BADO

Azam dhidi ya Yanga walianza na washambuliaji wawili Obrey Chirwa na Shabani Chilunda ambao walionekana kukosa umakini na kushindwa kutimiza majukumu yao ya kwanza ya kuweka mpira nyavuni licha ya kwamba mabeki wa Yanga walifanya makosa mengi.

Mastraika wa Azam Chirwa, Chilunda na Donald Ngoma ambaye aliingia baadaye walionekana kupata shida mbele ya Lamine Moro na Ally Sonso licha ya baadaye kuja kupewa kadi nyekundi lakini bado walionekana kucheza kama washambuliaji wa kawaida.

AZAM BILA MPIRA

Yanga wakati wanafanya makosa dhidi ya Azam ambao muda huo wakiwa hawana mpira walishindwa kuwafuata na kuwasukuma kwao ili kufanya makosa, bali walikuwa wakikaa nyuma na kuwasubiri wafike eneo lao.

Mara chache ambazo wachezaji wa Azam waliwafuata Yanga na kuwasukuma kwa nguvu katika eneo lao walipata mipira kuliko mara chache ambazo walishindwa kuipata.

MWAISABULA HUYU HAPA

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema Azam walionekana kuingia katika mchezo huo wakiifuatilia vya kutosha Yanga pindi wanapokuwa hawana mpira na pale wanapokuwa nao maana hata hawakupata shida kucheza nao.

“Yanga licha ya kwamba wamefanya usajili, lakini timu ilionekana kushindwa kucheza kwa kuelewana mbele ya Azam ambao walionekana kuimarika na kucheza vizuri huku wakifanya makosa ya mara kwa mara jambo ambalo wangecheza na timu yenye umakini katika kushambulia habari ingekuwa nyingine,” alisema Mwaisabula.