Yanga waita nyota wao wote

Muktasari:

Habari ambazo Mwanaspoti limezipata ni kwamba lengo la kikao hicho ni uongozi kutoa hatma ya wachezaji kiujumla.

UONGOZI wa klabu ya Yanga leo Jumatatu Agosti 3, 2020 watakutana na nyota wao wote kwa ajili ya kikao cha pamoja baada ya Ligi Kuu kumalizika.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo ambazo Mwanaspoti Online limezipata ni kwamba lengo la kikao hicho ni uongozi kutoa hatma ya wachezaji kiujumla kuelekea msimu ujao wa ligi kuu.

Imeelezwa kwamba Yanga inataka kupitisha panga la wachezaji katika kikosi chao na kubaki na wachezaji ambao wana amini kwamba wataisadia timu hiyo msimu ujao.

Pia katika kikao hicho kinawapa fursa wachezaji kutoa maoni yao kwa viongozi wao.

Mmoja wa wachezaji wa Yanga, ameitokeza Mwanaspoti Online kwamba kikao hicho kitafanyika leo asubuhi Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyopo mtaa wa Jangwa na Twiga, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

"Kweli tumeitwa leo asubuhi hapa najiandaa niende," amesema kwa kifupi.

Alipotafutwa Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ili kuzungumzia juu ya taraifa hizo lakini simu yake iliita bila kupokelewa.