Yanga waendelea na mazoezi, Morrison hajatokea

Muktasari:

Morrison wa Yanga aliondoka uwanjani jana baada ya kutolewa kwenye mechi dhidi ya Simba na nafasi yake ilichukuliwa na Patrick Sibomana.

WINGA Benard Morrison wa Yanga licha ya kuondoka jana uwanjani akiwa amepaniki, mchezaji huyo amekosekana katika mazoezi yanayoendelea leo Jumatatu jioni katika uwanja chuo cha Sheria, Mawasiliano.

Morison alitolewa katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Azam dhidi ya Simba na nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Sibomana lakini wakati anatoka alionekana kupishana maneno na muamuzi msaidizi.

Mwanaspoti ambalo limefika uwanjani hapo halikumuona kabisa mchezaji huyo katika mazoezi yanayoendelea.

Wakati Morison akiwa hayupo uwanjani hapo, wachezaji wengine ambao walicheza mchezo wa jana na hawakuwepo ni Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima,Metacha Mnata na Juma Abdul.

Alipoulizwa kuhusu kukosekana kwa wachezaji wake, kocha Luc Eymael alisema taarifa aliyonayo ni ya Papy Tshishimbi kwenda Hospitali.

"Sina taarifa  ya wachezaji kukosekana kwao hapa zaidi ya Tshishimbi" alisema kwa kifupi kocha huyo.

Wachezaji waliokuwepo katika mchezo wa jana na kucheza dakika 90, Jaffary Mohamed, Feisal Salum, Lamine Moro, David Molinga na Deus Kaseke wao walikuwa wanafanya mazoezi ya kunyoosha viungo kwa pembeni.

Wachezaji wengine waliokuwa wanafata programu ya mwalimu kocha Luc Eymael ni Faruk Shikhalo, Ramadhan Kabwili, Paul Godfrey, Tariq Seif, Ally Mtoni, Juma Mahadhi, Mrisho Ngassa, Yikpe Gnamien, Abdulaziz Makame, Mrisho Ngassa, Adeyum Saleh, Rafael Daud, Patrick Sibomana, Ditram Nchimbi na Eric Kabamba.

Hata hivyo mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi alichelewa kufika mazoezini baada ya kuchelewa dakika 46 wakati ambao Yanga wanaanza mazoezi saa 10:00 jioni na yeye alifika saa 10:46 jioni.

Alipofika alipewa programu ya kukimbia na baadaye aliungana na wachezaji wenzake.