Yanga sasa yapewa mashine ya mabao

Muktasari:

Safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoundwa na David Molinga, Juma Balinya, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob bado haijaonyesha makali yake vivyo hivyo kwa nyota wengine wazawa.

YANGA inapata tabu kusaka ushindi ndani ya uwanja. Matumaini ya mashabiki yameanza kupotea taratibu na sasa wameanza kumtolea uvivu Kocha Mwinyi Zahera wakidai, licha ya kukosa matokeo, lakini pia timu haichezi soka la kuvutia.

Wakati wa dirisha kubwa la usajili, Yanga ilionekana kufanya usajili wake kwa mipango ya chini kwa chini huku ikielezwa ni mapendekezo ya Zahera ambaye wakati huo alikuwa na kikosi cha Timu ya Taifa ya DR Congo kwenye fainali za Mataifa Afrika (Afcon) kule Misri.

Ilifumua karibu kila idara na kushusha wachezaji wa kigeni na wale wa ndani na kwa kuangalia rekodi za wachezaji waliosajiliwa, kila shabiki wa Yanga aliamini huu ni msimu wao.

Lakini, mambo yamekuwa tofauti na wakapoteza kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting kabla ya kulazimisha sare kwa Polisi Tanzania.

Katika mechi nne za Ligi Kuu Bara, Yanga imevuna pointi saba na mabao matano huku straika wa Simba, Meddie Kagere akifunga mabao saba peke yake. Yanga ilishinda dhidi ya Coastal Union bao 1-0, Mbao (bao 1-0), sare ya mabao 3-3 na Polisi Tanzania na ikachapwa na Ruvu Shooting bao 1-0.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoundwa na David Molinga, Juma Balinya, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob bado haijaonyesha makali yake vivyo hivyo kwa nyota wengine wazawa.

Molinga amefunga mabao mawili akiachwa nyuma kwa bao moja na Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania, ambaye aliipiga Yanga mabao matatu huku Miraji Athuman wa Simba akiwa na mabao manne.

Nchimbi mbali na kuonyesha makali yake Ligi Kuu Bara, lakini pia ameivusha Timu ya Taifa Tanzania, Taifa Stars kwenye Fainali za Chan baada ya rafu aliyochezewa kuzalisha bao la adhabu ndogo ya Erasto Nyoni kisha akafunga bao la ushindi dhidi ya Sudan jijini Khartoum.

Kwa sasa Yanga inaonekana kuwa imara zaidi kuanzia nyuma hadi eneo la kiungo huku ile ya ushambuliaji ikionekana butu na hapo ndipo ikashauriwa, Nchimbi anaweza kuwa suluhisho kama Yanga itamuangalia kwa jicho la pekee.

Pia, imetakiwa kwenda kumsajili beki kitasa wa Coastal Union ya Tanga, Bakar Mwamnyeto kwa ajili ya kuwa mbadala sahihi na wa muda mrefu wa beki, Kelvin Yondani, ambaye kwa sasa kilomita zake ni kama zimekata.

Kwa sasa Yondani, ambaye hivi karibuni alitangaza kustaafu kucheza soka la kimataifa akiwa na Nyoni, lakini Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akawarejesha akisema bado wana mchango mkubwa kwa Taifa Stars, ana miaka 35 na huenda asicheze soka la ushindani kwa muda mrefu hivyo Mwanyeto mwenye miaka 22 ni mtu sahihi.

Akizungumza na Mwanaspoti, staa wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amekiangalia kikosi cha Yanga ambacho kimetupwa nje ya Kombe la Shirikisho Afrika juzi kule Misiri, kisha akasema Nchimbi anaweza kuwa mkombozi ukilinganisha na waliopo sasa.

Alisema Yanga haina budi kuimarisha eneo la ushambuliaji kwa kunasa mtu mwenye uwezo wa kufunga na kulazimisha mashambulizi kwa wapinzani.

“Yanga inahitaji straika hatari ambaye muda wowote anaweza kufunga mabao, Simba ina Kagere ambaye anafanya vizuri kazi yake. Pia ina Miraji Athumani naye anafanya maajabu. Nchimbi yuko vizuri na anaweza kuwasaidia japo anahitaji kupigwa msasa kidogo tu,” alisema.

REKODI YA NCHIMBI

Kabla ya kutua Polisi Tanzania, Nchimbi aliichezea Majimaji aliyofungia mabao 15 misimu mitatu, alipotua Mbeya City kwa msimu mmoja alifunga mabao manane na asisti 12, na alipotua Njombe Mji alifunga mabao saba na asisti sita.

Mwanaspoti limezungumza na Nchimbi na kumuuliza kama Yanga itaamua kupiga hodi kutaka huduma yake ili kwenda kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji akasema:

“Nina malengo tofauti na wachezaji wengine. Natamani kufika mbali zaidi ya nilipotoka na ninapopata nafasi huwa siwazi mara mbili zaidi ya kufanya maamuzi magumu ili kufikia malengo na ndoto zangu.

“Najifunza kitu kikubwa sana kupitia Mbwana Samatta ambaye hakulewa sifa baada ya kutua Simba, akapata nafasi ya kucheza TP Mazembe na sasa Genk ambako imempa fursa ya kuweka rekodi kibao hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema.

WASIKIE HAWA

Mchambuzi wa soka nchini, Mwalimu Alex Kashasha alisema wachezaji wazawa kama Nchimbi wanaweza wakafanya makubwa kama wakisaidiwa.

Alisema wengi wana vipaji na uwezo mkubwa uwanjani, lakini wanahitaji kurekebishwa katika baadhi ya mambo machache ikiwemo kujitambua na kutovimba vichwa kwa mafanikio madogo yanayoanza kuchipuka kwao.

Alisema katika miaka ya 80 na 90, wachezaji wa kigeni alikuwa wachache kutokana na uwezo wa wazawa ambao, walionyesha soka maridadi kama kina Zamoyoni Mogella, Edibily Lunyamila na wengineo, akisisitiza walijitambua na kuuheshimu mpira.

“Kuna mechi moja niliiangalia ya Yanga, ilichezwa Uwanja wa Taifa, Kocha aliwaanzisha wachezaji wengi wa kigeni, timu ilikuwa haitembei ila alipoingia Deus Kaseke na Mapinduzi Balama timu ilianza kucheza soka la kasi, hilo tu linatosha kuwapa nafasi wazawa,” alisema Kashasha ambaye ni mchambuzi mahiri wa gazeti hili.

Pia, aliwashauri viongozi wa klabu za Ligi Kuu Bara kubadili mitazamo na kuwaamini wachezaji wazawa na kwamba, sio kila anayetoka nje ni mzuri.

“Wazawa wajifunze kujielewa waachane na mambo ya kivimba vichwa wanapong’aa mechi moja, mpira unahitaji heshima, wana nafasi kubwa ya kucheza Simba na Yanga, hivyo Nchimbi ajilinde ana kitu mguuni kwake,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha Kenny Mwaisabula alisema akitazama aina ya ucheze wa beki wa Coastal Union, Bakari Mwanyeto anaona ni mchezaji wa kwenda kuziba pengo la Yondani.

Alisema wakati Yanga inafanya usajili kwa ajili ya msimu huu, mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla alimwaeleza anamhitaji Mwamnyeto kwa hali na mali, lakini dili hilo lilikwama kwa kuwa hakuwa kwenye mipango ya Kocha Zahera.

“Msolla aliniambia anamhitaji Mwanyeto kwa sababu alikuwa ananishirikisha kwenye baadhi ya mambo kuhusu usajili, alipoona hayupo kwenye mipango ya Zahera akamuacha, lakini ni mchezaji anayetazamwa kwa jicho la tofauti,” alisema.

Alisema anaamini Wanayangwa atalifurahia dirisha dogo la usajili kwa kuwa, tayari Dk. Msolla ameanza kuwapa nafasi ya kuanza kufanya kazi ya kuibua na kuwafuatilia wachezaji wa kuwasajili.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema Mwanyeto ana faida mbili kama klabu hiyo itamsajili.

Kwanza ni umri mdogo akiwa na miaka 22 tu pamoja na kuendelea kupanda kwa kiwango chake.

“Yanga ikiamua kuwa na utaratibu wa kuwachukua vijana wa kuwa mbadala wa wachezaji wameanza kuchoka basi watakuwa na timu ya maana na yenye ushindani.

“Wakimsajili dirisha dogo naamini ataanza taratibu kujengewa uzoefu kwani, aina yake ya uchezaji ni mtu sahihi ambaye atakuja kuziba pengo la Yondan akistafu,” alisema.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwamnyeto alisema soka ni kazi yake hivyo hawezi kuchagua mahali kwa kufanya kazi kama Yanga itafuata taratibu yeye yuko tayari.