Yanga noma ... yavuta jembe lingine

Monday December 10 2018

 

By Thomas Ng'itu

MABOSI wa Yanga wameichungulia Simba na Azam na kubaini kuwa, wana majembe ya hatari na ili kula nao sahani moja katika mbio za ubingwa ni lazima waongeze vifaa vya maana vya kuweza kuwakimbiza mchakamchaka wapinzani wao.

Na fasta wakakubalina kwa pamoja na benchi la ufundi kuhakikisha wanafanya usajili matata wa vifaa vitatu vya maana, mbali na winga Ruben Bomba, huku jina kubwa katika usajili huo wa kufungia mwaka ukimlenga straika machachari, Umar Kasumba.

Mabosi hao wa Yanga wanapambana kuhakikisha wanafanya maboresho ya kikosi chao katika mkakati wa siri, lakini jina la straika huyo mpya Mganda kila mmoja amelikubali na wameafikiana lazima atue Jangwani.

Kasumba anatakiwa na Kocha Mwinyi Zahera aliyesisitiza mapema anataka mshambuliaji mwenye nguvu atakayecheza sambamba au nyuma kidogo ya straika wake wa sasa Heritier Makambo.

Chaguo lao la kwanza likatua kwa Kasumba anayekipiga Klabu ya Sofapaka ya Kenya na wakati wowote mambo yakikaa sawa atavaa jezi ya Donald Ngoma yaani namba 11 ambaye alivunjiwa mkataba na kukimbilia zake Azam FC.

Kwa sasa inaelezwa mabosi wa Yanga wanapambana na mmiliki wa Sofapaka, Elly Kalekwa ili kuhakikisha wanamchukua mshambuliaji huyo aje kuiongezea nguvu timu yao iliyokuwa uwanjani usiku wa jana Jumapili kuvaana na Biashara United ya Mara.

Hata hivyo, jaribio la Yanga kumfuata Kasumba linakuwa ni kwa mara ya pili kufuatia awali tajiri mmoja wa Yanga kujaribu kuongea na Kalekwa kumnunua mshambuliaji huyo lakini mmiliki huyo wa aliweka ngumu kumuuza.

Endapo Yanga itamnasa Kasumba klabu hiyo itakuwa imelamba dume kwani mshambuliaji huyo huwa hakubali kuzuiwa kirahisi hata na mabeki wabishi.

Mbali na Kasumba, Yanga pia inasaka mshambuliaji mwingine wa ligi ya ndani ikisubiri uamuzi wa Kocha Zahera anayefuatilia, japo Mwanaspoti linafahamu pia Jangwani inampigia hesabu Charles Ilanfya wa Mwadui FC ili imbebe.

KASUMBA NI NOMA

Straika huyo mwenye umri wa miaka 24, akiwa amezaliwa mwaka 1994 kule kwao Uganda, alianza kufahamika kisoka mwaka 2013 alipojiunga na Polisi Uganda na kufanya mambo makubwa katika kucheka na nyavu kabla ya Majogoo wa Kampala, SC Villa kumbeba na kuichezea kwa mafanikio hadi mwaka jana alipotua Sofapaka na kuwakimbiza Wakenya kwa umahiri wake wa kutupia kambani.

Ni mshambuliaji mrefu wa kimo cha Mita 1.81 na uzito wa kilo 72 anasifika kutumia miguu yote.

Kasumba pia ana uwezo mkubwa wa kunusa goli lilipo kama haitoshi ana mbio za kutosha na anapiga chenga na mjanja wa kuwasumbua mabeki na uwezo wake mkubwa wa kufumua mashuti ambayo yamekuwa yakiwatesa makipa katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Advertisement