Yanga na Simba mbio za ubingwa, Biashara United wagoma kushuka daraja

Wednesday March 13 2019

 

By Saddam Sadick

MWANZA. BIASHARA United juzi iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda, lakini benchi la ufundi la timu hiyo limeibuka na kutamka mbele ya mashabiki wao kwamba ishu ya kushuka daraja kwao haipo, hivyo wawe na imani na timu yao kuiona msimu ujao wa Ligi Kuu.

Pamoja na ushindi huo, lakini bado wamebaki nafasi ya 19 kwenye msimamo wakiwa na pointi 27  huku African Lyon wakiendelea kushika mkia wakiwa na alama 22.

Biashara United ili ijihakikishia kubaki kwenye ligi msimu ujao itahitaji ushindi wa mechi nne mfululizo.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Omary Madenge alisema licha ya hali mbaya waliyonayo lakini wamejidhatiti vyema hivyo mashabiki na wadau wa soka mkoani Mara wasiwe na presha ya kushuka daraja.

Alisema mkakati wao ni kila mchezo kuvuna pointi tatu na kwamba Ligi imekuwa ngumu ila wamewaandaa kisaikolojia nyota wao kupambana bila kukata tamaa hadi kufikia malengo.

"Tunashukuru kwa ushindi lakini niwaambie mashabiki wetu waendelee kutupa sapoti tu, timu itabaki Ligi Kuu tumeazimia kila mchezo kwetu ni pointi tatu,” alisema Madenge.

Nahodha wa timu hiyo, Abdulmajid Mangalo alisema kipindi hiki hawana muda wa kupoteza zaidi ya kujiandaa vyema kila mechi iliyo mbele yao, kwani ligi inakwenda kwa kasi hivyo ni lazima wahakikishe wanainusuru timu yao.

Aliwataka wachezaji wenzake kila mmoja kujituma na kusahihisha makosa waliyoyafanya mechi zilizopita ili kupata ushindi kwenye michezo iliyobaki.

“Kwa sasa ni kupambana jihadi kwa mechi zilizobaki na jambo la kila mchezaji kuonyesha uwezo wake hasa mechi zilizobaki ili kupata ushindi na kuinusuru timu kutoshuka daraja,” alisema Mangalo.

Timu za Simba, Yanga na Azam FC zimekuwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ambapo hadi sasa timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani ndiyo inaongoza Ligi Kuu ikiwa na alama 67.

Azam inafuatia nafasi ya pili ikiwa na pointi 53 ikifuatiwa na Simba kwenye nafasi ya tatu ikiwa imekusanya alama 51.

 

 

Advertisement