Yanga mpya nyuma chuma mbele wembe

Tuesday July 16 2019

 

By Charity James

DIRISHA la usajili kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na La Pili litafungwa Julai 31.

Mpaka sasa kuna baadhi ya klabu zimekamilisha usajili kwa kunasa vifaa matata ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 23, sambamba na michuano ya kimataifa.

Klabu za Simba, Yanga, Azam FC na KMC ndizo zitakazoshiriki michuano ya kimataifa msimu ujao na kila moja imeshafanya usajili wake, huku baadhi zikiwa zimeshatuma majina ya vikosi vyao kwenye ofisi za CAF.

Yanga yenyewe imeshatuma jeshi lake likiwa na nyota wapya 13, sambamba na wale wa msimu uliopita ambao watakuwa na kazi moja mbele ya Kocha Mwinyi Zahera kufanya mambo ili timu itishe.

Mwanaspoti limekuchambulia nyota hao wapya 13 walioungana na wale wa zamani kikosi na kuendelea kujifua kwenye kambi ya mazoezi mjini Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kujipima nguvu na kutambulishwa rasmi Agosti 4, jijini Dar es Salaam.

MAKIPA KAZI IPO

Advertisement

Ilikuwa ni vigumu kwa Bandari Kenya kumwachia kipa wake, Farouk Shikalo lakini kutokana na nguvu ya Yanga, Shikalo ametua Jangwani. Hata hivyo, katika nafasi hiyo ya kipa, msimu uliopita alisimama Klaus Kindoki aliyeisaidia Yanga akishirikiana na Ramadhani Kabwili kumaliza nafasi ya Pili. Kindoki aliaminiwa na Zahera baada ya aliyekuwa kipa namba moja, Beno Kakolanya kuzinguana na uongozi kwa madai ya mshahara wake.

Kindoki sasa ameongezewa changamoto mpya kwa kusajili Shikalo na kwa mujibu wa mkataba wake, atakuwa kipa namba moja.

Yanga pia imemsajili kipa wa Mechata Mnata na atakuwa akisubiri benchi kusubiri atakayeumia achukue nafasi yake na kama ataweza kumshawishi Kocha Zahera anaweza kuwapa changamoto Shikalo na Kindoki.

MABEKI NAKO MOTO

Katika usajili wa msimu huu, Yanga imevuta jumla ya mabeki watano ambao ni watu wa kazi na mwunganiko wao na wale wanaowakuta, moto utawaka Jangwani.

Yanga imemsajili Ali Ali ‘Mwarabu’ kutoka KMC, ili atoe changamoto kwa mabeki. Msimu uliopita nafasi ya beki namba mbili ilikuwa ikitumiwa na chipukizi Paul Godfrey ambaye alimweka benchi mkongwe, Juma Abdul kutokana na uwezo wake wa kupanda na kushuka uliomshawishi Kocha Mwinyi Zahera kumpa namba kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, kutokana na presha ya michuano ya kimataifa huku Yanga ikipania kufikia au kuzidi mafanikio ya watani zao Simba, Zahera ameamua kumleta Ali kumpa changamoto Paul Godfrey.

Beki Gadiel Michael ametimkia Msimbazi, lakini mabosi wa Yanga walimsainisha Mharami Issa ‘Marcelo’ ili kuziba nafasi yake akitokea Malindi ya Zanzibar, japokuwa alishatangazwa na Singida United.

Marcelo atakuwa na kazi ya kushirikiana na Ally Mtoni ‘Sonso’ kwani beki huyo kutoka Lipuli licha ya kumudu beki ya kati lakini anacheza pia pembeni.

Kama Sonso anasalia kati atapambana na kina Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondani ambaye ndiye alikuwa akiongoza safu ya ulinzi kutokana na ubora wake ikiwa ni sambamba na ukongwe kwenye ligi hiyo.

Pia, kuna Mghana Lamine Moro kwa ajili ya kumsaidia Yondani katika majukumu yake na atasaidiwa pia na beki mwingine wa kati, Selemani Mustafa aliyesajiliwa akitokea Aigle Noir ya Burundi kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani na ana uwezo pia wa kucheza kama kiungo mkabaji. Hii ni kuonyesha eneo la ulinzi Yanga litakuwa matata kwelikweli.

VIUNGO/WINGA

Kwenye eneo la kati na pembeni mbele, mabosi wa Yanga wametumia akili kubwa kunasa wakali watatu matata wa kusaidia na wachezaji waliobakishwa kwenye kikosi cha msimu uliopita.

Yanga imesajili viungo wanaoumudu pia kucheza kama mawinga ambao ni Abdulaziz Makame, Patrick Sibomana na Mapinduzi Balama.

Jeshi hilo linaungana na kina Papy Kabamba Tshishimbi, Feisal Salum, Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Rafael Daud na wachezaji wengine kutoka kikosi cha vijana waliokuwapo msimu uliopita na wale waliopandishwa msimu huu.

Balama amejiunga na Yanga akitokea Alliance FC na alikuwa na msimu mzuri akiwa katika kikosi hicho akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na kuwavutia matajiri wa klabu hiyo na kumvuta fasta. Huku Makame akitokea Mafunzo ya Zanzibar akicheza kama kiungo mkabaji kuifanya safu ya kiungo kuwa imara zaidi. Pia, imemsajili winga hatari akitokea Mukura Victory Sports ya Rwanda, Patrick Sibomana atakayekuwa na kazi ya kupandisha mashambulizi.

Nafasi ya Issa Bigirimana aliyetokea APR ya Rwanda pamoja na mawinga wazoefu, Ngassa na Kaseke, Daud na Mohammed Issa ‘Banka’ wakifanya kazi zao kwa ufanisi ni wazi mashabiki wa Yanga wanaweza kabisa kumsahau Ibrahim Ajibu aliyerejea Msimbazi.

HUKO MBELE BALAA

Kama kuna kitu ambacho mashabiki wa Yanga wanakisubiri ni kutaka kuona safu ya mbele ya klabu hiyo msimu huu itakuwaje, maana msimu uliopita iliyumba sana na kumtegemea zaidi Heritier Makambo aliyetimkia Guinea.

Makambo ndiye aliyekuwa mfungaji tegemeo, japo Amissi Tambwe, Ajibu na kina Ngassa nao walikuwa na mchango, lakini kitendo cha mabosi wa Yanga kuvuta washambuliaji wakali kwa mpigo kumewashtua hata wapinzani wao.

Yanga imemsajili Juma Balinya aliyemaliza Ligi Kuu ya Uganda msimu uliopita akifunga mabao 19 na kuwa Mfungji Bora, lakini pia ina Maybin Kalengo kutoka Zambia alikokuwa akiiichezea Zesco United na pia ina Mnamibia, Sadney Urikhob.

Balinya ndiye anayetajwa kama mrithi wa kuziba wa Makambo, huku kina Urikhob, Kalengo na hata Birigimana na Sibomana ambao pia wanamudu safu ya ushambuliaji wakisubiriwa kuwazika jumla kina Tambwe na Ajibu.

Washambuliaji hao watakuwa na kazi moja tu ya kutupia kambani ili kuibeba Yanga katika mechi za Ligi Kuu, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika watakaoshiriki baada ya CAF kuiongezea nafasi Tanzania ya kuwakilishwa na timu mbili sawa na ilivyo kwenye Kombe la Shirikisho ambapo jukumu litakuwa kwa Azam na KMC.

Advertisement