Yanga mpya ni wafungaji, mabeki tu

Muktasari:

Msimu mpya wa Ligi Kuu Bara umepangwa kuanza Septemba 6 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jana jioni.

Dar es Salaam. Ikionyesha kuwa imepania kufanya vizuri msimu ujao, Yanga imeshauriwa kufanya marekebisho katika safu ya ushambuliaji na ulinzi ili kurudisha makali yake.

Yanga imetakiwa kusajili wachezaji wenye uwezo binafsi kama ilivyo kwa wapinzani wao wakubwa, Simba na kuongeza nguvu kubwa kwenye eneo la ushambuliaji, ambalo ndilo lililowagharimu msimu huu.

Yanga imewaacha nyota wake 14, ambao ni Mrisho Ngassa, David Molinga, Andrew Vincent, Papy Kabamba Tshishimbi, Jafary Mohammed, Tariq Seif na Mohammed Issa ‘Banka’, ambao mikataba yao imemalizika.

Wengine ambao wapo katika mazungumzo ya kuvunjiwa mikataba ni Ali Mtoni Sonso, Muharami Issa, Ali Ali, Yikpe Gislain, na Patrick Sibomana ambaye tayari amewaaga mashabiki wa Jangwani.

Timu hiyo imebakiza nyota 14, ambao ni Faroukh Shikalo, Ramadhan Kabwili, Metacha Mnata, Feisal Salum, Juma Mahadhi, Adeyum Saleh, Said Makapu, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke, Ditram Nchimbi, Abdullaziz Makame, Paul Godfrey na Bernard Morrison, lakini ikiendelea na mazungumzo na wakongwe wawili Juma Abdul na Kelvin Yondani, ambao mikataba yao imeisha.

Kilichoiponza Yanga

Yanga iliponzwa na udhaifu wa kikosi chao kwani ilikuwa na wachezaji wengi wazuri wanaoanza, lakini wengi waliobaki benchi walikuwa si aina ya wachezaji wanaoweza kubadili matokeo na kuibeba timu.

Wachezaji wengi wa kikosi hicho walikuwa na viwango vya kawaida huku safu ya ushambuliaji ikionekana kupwaya zaidi na Molinga ndiye aliyeonekana angalau anaibeba timu hiyo kwa mabao yake 11 aliyofunga.

Yanga tayari imeshaanza kuiimarisha safu ya ushambuliaji baada ya kuinasa saini ya mshambuliaji wa Mbao FC, Waziri Junior aliyefunga mabao 13 kwenye ligi.

Maeneo ya kuboresha

Mchambuzi wa soka na nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema timu hiyo ingeweza kuwaacha wachezaji wengi zaidi ya hao 14 kipindi hiki.

“Kuna kigezo kikubwa kinatumika katika kumuacha au kusajili mchezaji, katika soka kocha ni mtu pekee anayewafahamu wachezaji kuliko hata ambavyo wenyewe wanajifahamu,” alisema Mayay.

Alisema klabu hiyo inapaswa kuwa na aina ya wachezaji wenye uwezo binafsi kama ilivyo kwa wachezaji wa Simba, ambayo ni mshindani wake katika soka la Tanzania.

Kauli ya kiungo huyo wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa imeungwa mkono na nyota mwingine wa zamani wa Stars, Peter Tino, ambaye alisema katika suala la klabu kumuacha mchezaji kuna vitu vingi vinaangaliwa.

“Wakati mwingine mchezaji anaweza kufanya vizuri kwenye mechi fulani, lakini akaachwa, watu wanahoji, lakini wanasahau sifa ya mchezaji sio kucheza tu uwanjani, kuna vitu vingi vya kuangaliwa,” alisema.

Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisema kuachwa kwa wachezaji hao ni jambo la kawaida kwa harakati za kuboresha kikosi, lakini akashauri kuwa wanapaswa kuongeza nguvu zaidi katika safu ya ushambuliaji kwenye usajili mpya.

“Pia, kwenye nafasi ya viungo washambuliaji, wasimtegemee zaidi Niyonzima (Haruna), japo kila idara inahitaji kufanyiwa maboresho, ila mapungufu makubwa yako eneo la ushambuliaji,” alisema Mmachinga.

Licha ya Yanga kumsajili Junior katika kuimarisha safu ya ushambuliaji, Mayay alisema kinda huyo ni mapema kumvalisha viatu vya waliowahi kuwa washambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo au Amis Tambwe.

Kipa wa zamani wa Yanga aliyeichezea timu hiyo miaka ya 1980, Hamis Ramadhan alisema timu hiyo haitakiwi kufanya tena makosa katika usajili wa wachezaji wake ili isije kuwagharimu kama ilivyokuwa msimu uliopita.