Yanga kuweni makini na wachezaji hawa wa Zesco

Muktasari:

Zesco imejengwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa, ambao Yanga wanapaswa kuwa makini nao kwa dakika zote tisini ili kuanza vyema safari yao ya kwenda hatua ya makundi

Dar es Salaam. JUMAMOSI hii Yanga itashuka katika Uwanja wa Taifa katika mchezo wake wa hatua ya pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia, kutafuta tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi hiyo.

Yanga ilifika hatua ya pili baada ya kulipiza kisasi kwa kuwaondosha Township Rollers kwa mabao 2-1 katika michezo yote miwili ya Ligi hiyo. Township iliwahi kuiondosha Yanga misimu miwili iliyopita.

Mchezo huo unatazamiwa kuwa wa aina yake na wakipekee hasa kutokana na timu hiyo kuwa ndiyo pekee kutoka nchini inayoshiriki michuano hiyo baada ya watani wao Simba kutolewa na UD Songo wiki mbili zilizopita.

Yanga imekuwa ikitumia vyema michezo ya maandalizi katika ziara yao waliyofanya hivi karibuni kanda ya ziwa kwa lengo la kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa.

Katika ziara hiyo Yanga imecheza michezo miwili, dhidi ya Pamba Fc mchezo uliosiha kwa sare ya 1-1 na dhidi ya Toto African ulioisha kwa Yanga kushinda mabao 3-0, huku mshambuliaji wao mpya David Molinga akibuka kidedea kwa kufunga mabao mawili katika mchezo huo.

Pamoja na hilo, wapinzani wao Zesco sio wabaya kwani hata katika michezo mitatu waliyocheza msimu huu wameshinda yote licha ya kwamba ni kwa ushindi mwembamba.

Katika mchezo wao wa kwanza wa ligi walishinda bao 1-0 dhidi ya Zanaco na kushinda tena mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Green Mamba Fc kwa mabao 3-0 katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.

Zesco imejengwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa, ambao Yanga wanapaswa kuwa makini nao kwa dakika zote tisini ili kuanza vyema safari yao ya kwenda hatua ya makundi. Hawa ndiyo wachezaji watano tishio ambao Yanga wanapaswa kuhakikisha wanawachunga kwa dakika zote.

JESSE WERE

Huyu ni mshambuliaji raia wa Kenya katika misimu yake miwili akiwa na Tusker ya nchini kwao alifunga mabao 34, katika michezo yote baada ya kujiunga na Zesco 2016, ameendelea kuwasha moto. Chini ya kocha George Lwandamina, Were amekuwa chaguo la kwanza na mwenye kuaminika.

Sifa za mchezaji huyo aliyewahi kutakiwa na Kaizer Chief, ana kasi ya ajabu na mwepesi wa kufanya maamuzi ndani ya eneo la hatari, Yanga inapaswa kuwa makini na mchezaji huyo aliyefunga bao pekee katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Green Mamba Fc.

UMARU KASUMBA

Ukiwa ni msimu wake wa kwanza katika kikosi hicho, Kasumba ameanza vizuri kwa kufunga bao moja katika mchezo wa marudiano kufuzu Ligi ya Mabingwa dhidi ya Green Mamba Fc. Kasumba mwenye umri wa miaka 25 ni mrefu mwenye sentimita 181 ni mzuri kwa mipira ya vichwa hivyo Yanga wanapaswa kuhakikisha hawaruhusu ukigwaji wa krosi.

Msimu wa 2018/2019 alishika nafasi ya tatu kwa ufungaji bora baada ya kufunga mabao 17, baada ya msimu kumalizika alipata ofa ya kwenda kufanya majaribio nchini Ujerumani na kushindika na kuangukia Zesco United baada ya Nkana Fc kumkosa ambao pia walikuwa wakimuhitaji.

JOHN CHING’ADU

Kiungo huyu mshambuliaji raia wa Zambia ni mzuri kwenye kupiga mashuti yenye macho, pamoja na kugawa pasi za mwisho awapo uwanjani, ni mchezaji ambaye kila kona ya uwanja unamuona katika kuhakikisha anasaidia timu yake.

Yanga wanapaswa kuhakikisha mchezaji huyo hapigi shuti lolote na wala kutoa pasi ya mwisho inayoweza kuleta madhara kwa upande wao. Kiungo huyo alifunga bao moja katika mchezo wa kufuzu Ligi ya Mabingwa dhidi ya Green Mamba Fc.

MARCEL KALONDA

Beki huyo wa kati raia wa Congo, sifa kubwa aliyonayo ni upigaji wa vichwa, hii inatokana na urefu alionao unakadiriwa kufika sentimita 188, njia pekee ya kumzuia, Yanga wanapaswa kuhakikisha hawaruhusu kona au mpira ya adhabu na kumkaba muda wote na kuhakikisha haruki.

Kalonda ni mchezaji pekee mdogo 21, kwenye kikosi hicho na kocha Lwandamina ameonyesha kuwa na imani naye katika michezo miwili iliyopita na mmoja wa ligi uliopigwa wiki tatu zilizopita dhidi ya Zanaco.

ENOCK SABUMUKAMA

Alifunga bao pekee kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Zanaco, sifa kubwa ya mchezaji huyo ni kumiliki mpira na kutoa pasi za uhakika kwa wakati sahihi.

Yanga inapaswa kuhakikisha hawamruhusu kiungo huyo kumiliki mpira kwa muda mrefu kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanampa faida ya kupenyeza pasi kwa uhakika hali itakayoweza kuwagharimu.