Yanga kunoa makali kwa Namungo FC

Muktasari:

Wakati timu zikiwa kwenye mapumziko kupisha mechi ya Taifa Stars na Lesotho, kikosi cha Yanga kinatarajia kwenda Ruangwa mkoani Lindi kucheza mechi ya kirafiki na Namungo FC ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuivaa Mwadui FC.

Dar es Salaam. Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam Novemba 17, kwenda Ruangwa mkoani Lindi, baada ya kupewa mwaliko maalumu na Mbunge wa jimbo hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na watakapokuwa huko wamepanga kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namungo FC.

Akizungumza na MCL, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaaya amesema wanafurahia mwaliko huo kwa sababu unawapa fursa ya kujiandaa zaidi kuelekea mchezo wao wa kiporo dhidi ya Mwadui FC.

"Ni kweli tuna mwaliko kutoka kwa Mh, Majaliwa, tumekubali kwenda jimboni kwake tukifika huko tarehe 18, tutacheza na Namungo baada ya mchezo tutakuwa na mapumziko na kesho yake tutarudi Dar es Salaam. Baada ya hapo tutaungana na wachezaji wengine waliokuwa na Taifa Stars tayari kwa mchezo wetu na Mwadui FC," alisema Kaaya.

Amesema mbali na mwaliko huo leo Jumamosi wanatarajia kushuka dimbani kukipiga na African Lyon mchezo unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dra es Salaam na Jumatano watacheza na Reha.

Yanga itacheza na Mwadui FC mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao walishindwa kucheza kutokana na kukabiliwa na mashindano ya kimataifa.