Uongozi wa Prisons waivimbia Yanga

Wednesday December 6 2017

 

By Justa Musa

Mbeya. Ndoto ya Klabu ya Yanga kumnasa nyota wa Tanzania Prisons, Mohamed Rashid huenda isitimie baada ya uongozi wa klabu yake anayotumikia sasa kusema haendi popote.
Mohamed ambaye aliushawishi uongozi wa Yanga kwa kuwa na kipaji kizuri cha uchezaji pamoja na kufumania nyavu,amekuwa akiinyima usingizi klabu hiyo ambayo ilitangaza kumng’oa kwa gharama yoyote ile  lakini ‘dili’ hilo limekwama.
Katibu wa Prisons, Havintish Abdallah alisema kwamba hawawezi kumruhusu mchezaji huyo kwenda katika klabu yoyote kwani bado ni mchanga katika soka.
Alisema hata ikitokea klabu inataka kumsajili kwa gaharama yoyote lakini uongozi hauwezi kukubali kumuachia kirahisi rahisi kwani bado wanamhitaji katika kuipigania timu.
Alisema ‘Hatuwezi kumpeleka mchezaji ambaye tunaona kabisa atakwenda kupata changamoto kwani  klabu zetu hizi kongwe zinatamani tu kumtoa sehemu na kumpeleka sehemu halafu wasimtumie’.
Havintishi alisema bado Prisons inamhitaji na inataka kumuona akiendelea kuwa mwiba kwa timu pinzani kila wanapokutana nao na hatimaye aweze kutimiza ndoto zake za ufugaji bora anazofukuzia.
Kwa upande wake mchezaji huyo aliyefikisha idadi ya mabao sita hadi sasa alisema yeye ni mali ya Prisons na kwamba maamuzi yote yatabaki katika uongozi wake uliochukua na kumthamini kwa kumsajili.
Mchezaji huyo anashika nafasi ya pili katika ufugaji bora huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na Mganda Emmanuel Okwi ambaye amefikisha mabao nane.