Yanga kumbe haiwezi Simba buana!

Muktasari:

Kipigo hicho kilichopatikana kwenye Uwanja wa Karume, ni cha pili kwa Yanga Princess mbele ya watani wao, kwani katika mchezo wa duru la kwanza wa ligi hiyo, Jangwani waliochakazwa mabao 7-0 na kufanya msimu wao wa kwanza mbele ya Msimbazi kupigwa mabao 12-1.

YANGA haiwezi Simba buana! Achana na Ligi Kuu Bara ya Wanaume ambapo Yanga ilicharazwa bao 1-0 Februari 16 na Simba kwa bao la Meddie Kagere, imedhihirika msimu huu Yanga yote haiwezi Simba baada ya jioni hii Yanga Princess kuchakazwa mabao 5-1 na Simba Queens katika Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL).
Kipigo hicho kilichopatikana kwenye Uwanja wa Karume, ni cha pili kwa Yanga Princess mbele ya watani wao, kwani katika mchezo wa duru la kwanza wa ligi hiyo, Jangwani waliochakazwa mabao 7-0 na kufanya msimu wao wa kwanza mbele ya Msimbazi kupigwa mabao 12-1.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali, huku Yanga Princess ikionekana kuimarika tofauti na mechi yao ya duru la kwanza, mabao ya washindi waliwekwa kimiani na Opah Clement aliyetupia mawili kambani, huku Mwanahamisi Omary 'Gaucho', Joele Bukulu na Amina Ramadhani kila mmoja akifunga moja.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha alama 34 baada ya mechi 16 , ingawa jioni hii pia kulikuwa na mechi nyingine nne za ligi hiyo na Mwanaspoti Online itakuletea matokeo yote kwa ujumla baadaye kujua nani amepanda na kushuka wapi katika msimamo huo, ingawa JKt Queens ubingwa kwao upo wazi kutokana na kushinda mfululizo tangu msimu uanze ikiongoza kileleni.