Yanga kukaa kileleni yazitesa timu vigogo Kanda ya Ziwa

Muktasari:

Mwadui iliyocheza mechi 33 hadi sasa, imevuna pointi 37 na kukaa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na Yanga wenye alama 74 na kuifanya timu hiyo kuhitaji pointi za ziada ili kubaki msimu ujao.

MWANZA. WAKATI timu za Kanda ya Ziwa zikiwa katika hatari ya kushuka daraja, Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu amekiri kuwa mambo ni magumu huku akisema mechi tano zilizobaki kwao ni kucheza kufa na kupona ili wabaki kwenye ligi kuu.

Mwadui iliyocheza mechi 33 hadi sasa, imevuna pointi 37 na kukaa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na Yanga wenye alama 74 na kuifanya timu hiyo kuhitaji pointi za ziada ili kubaki msimu ujao.

Bizimungu alisema kutokana na hali ilivyo, kipindi hiki ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake kujituma kuhakikisha ushindi unapatikana nyumbani na ugenini.

“Hatushuki daraja sema Ligi imekuwa ngumu zaidi na inatubidi kupambana sana hasa mechi zilizobaki, kila timu inahitaji ushindi kwa kila mchezo bila kujali wapo uwanja gani,” alisema Bizimungu.

Kocha huyo alisema baada ya mechi yao na Lipuli waliyoambulia sare ya mabao 2-2 waliendelea na maandalizi kuhakikisha makosa aliyoyaona mechi iliyopita yanafanyiwa kazi.

Alisema moja ya mapungufu aliyobaini hadi sasa ni safu yake ya ushambuliaji kutokuwa makini wawapo eneo la hatari pamoja na beki kutokuwa makini kulinda ushindi.

“Tunaendelea na mazoezi kwa ajili ya michezo yetu ijayo, natakiwa kufanya marekebisho makosa yalionekana katika michezo iliyopita. Tunataka kuhakikisha tunabaki kwenye ligi msumu ujao,” alisema.