Yanga kuingia kambini Agosti 10

Muktasari:

Yanga mpaka sasa imefanikiwa kusajili nyota wanne pekee huku ikiwafungashia vilago 14 kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho kuelekea msimu ujao

LICHA ya kutokuwa na benchi la ufundi na wachezaji wa kutosha mpaka sasa, baada ya kuwatimua nyota 14, Klabu ya Yanga imetangaza kuingia kambini rasmi Jumatatu Agosti 10, 2020.

Hadi sasa Yanga ndiyo klabu ambayo imeachana na wachezaji wengi baada ya dirisha la usajili kutangazwa Agosti Mosi kuliko klabu zingine za Ligi Kuu, wakiwa na lengo la kuboresha kikosi chao kiweze kuleta ushindani zaidi msimu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa klwenye ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Instagram wa klabu hiyo, timu ya Wananchi itaingia kambini kuanza maandalizi ya msimu mpya unaotarajiwa kuanza Septemba 6.

Yanga msimu ujao haitakuwa na uwakilishi wowote wa kimataifa baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu na FA ambao wote umetwaliwa na watani zao Simba.

Wachezaji wanne waliosajiliwa na kutangazwa rasmi na Yanga mpaka sasa ni Wazir Junior kutoka Mbao, Bakari Mwamnyeto kutoka Coastal Union, Zawadi Mauya kutoka pamoja Kagera Sugar na Yassin Mustapha kutoka Polisi Tanzania wachezaji wote wakiramba kandarasi ya miaka miwili.

Nyota walioachwa huru ndani ya kikosi hicho ni Mrisho Ngasa, David Molinga, Jaffar Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vicent, Papy Kabamba na Mohamed Banka.

Waliovunjiwa mikataba ni Ally Mtoni, Muharan Issa, Ali Ali, Yikpe Gislain, Patric Sibomana, Erick Kabamba pamoja na Rafael Daud.

Huku waliobaki ndani ya kikosi hicho Farouk Shikhalo, Ramadhan Kabwili na Metacha Manata.

Wengine ni Haruna Niyonzima, Lamine Moro, Benard Morrison, Juma Mahadhi, Feisal Salum, Adeyun Salehe, Said Makapu, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke, Ditram Nchimbi, Abdulaziz Makame na Paul Godfrey.