Yanga ina vigogo zaidi ya 100 mjue

Muktasari:

Hata hivyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumburi amefafanua hilo kwa kudai kila kamati ina kazi zake na ni vigumu kuingiliana. Pia anadai wala sio ajabu kuwepo kwa utitiri huo wa kamati Yanga.

MABINGWA wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga wametia fora baada ya kuwa na kamati nyingi tangu uongozi mpya wa Dk Mshindo Msolla uingie madarakani, ambapo mpaka unaposoma taarifa hii wanazo kamati nane zinazojumuisha wajumbe zaidi ya 100.

Utitiri huo wa kamati umeibua mijadala kwa baadhi ya wadau wa soka wakihofia huenda kamati hizo zikaingiliana kiutendaji, pia kuwepo kwa uvujaji wa taarifa mbalimbali za klabu hiyo kama viongozi wa juu hawatakuwa makini.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumburi amefafanua hilo kwa kudai kila kamati ina kazi zake na ni vigumu kuingiliana. Pia anadai wala sio ajabu kuwepo kwa utitiri huo wa kamati Yanga.

KIKOSI KAZI

Siku chache zilizopita Kamati ya Utendaji ya Yanga ilimteua Rodgers Gumbo ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ambayo inajumuisha wajumbe 13.

Katika orodha hiyo yupo Hersi Said, Beda Tindwa, Thobias Lingalangala, Edward Urio, Max Komba, Salum Mkemi, Yossuphed Mhandeni, Yanga Mkaga, Adonis Bitegeko, Heriel Mhulo, Issack Usaka, Deo Muta na Hassan Hussein.

Wiki iliyopita Saad Khimji ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Matawi ya Wanachama yenye wajumbe 10 ambao ni pamoja na Hamis Msumi, Hamis Kinye, Hassan Hussein, Abdallah Chikawe, Edward Mhagama, James Nhende, Mwantumu, Mgonja, Devotha Mkemwa, Samwel Koroso na Denis Mugisha.

Mbali na kamati hiyo tayari kulikuwa na Kamati ya Usajili chini ya mwenyekiti Franck Kamugisha akisaidiwa na Ahmad Islam, Samwel Rupia, Rogers Gumbo, Samwel Luqumay, Moses Katabaro, Abdallah Bin Kleb na Lucas Mashauri

Pia ipo Kamati ya Hamasa na Uchangiaji yenye watu watatu ambao ni Ivan Tarimo, Leavan Maro na Richard Kalongola ambayo iliundwa ili kuongeza nguvu katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

JESHI LAONGEZWA

Julai Mosi mwaka huu, iliundwa Kamati ya Fedha na Mipango yenye watu 10 ambayo ipo chini ya Arafat Haji kama mwenyekiti akisaidiwa na Makamu Shija Richard na Deo Mutta akiwa katibu, wajumbe wake wakiwa ni Said Kambi, Ally Mayay, Pindu Luhoyo, Baraka Katemba, Suma Mwaitenda, Haruna Mwaitenga na Ivan Tarimo.

Kadhalika Yanga ina Kamati ya Sheria na Nidhamu yenye watu tisa ikiongozwa na Sam Mapande huku wajumbe wakiwa ni Esther Cheyo, Shafiru Maakosa, Shabani Mgonja, Benjamin Mwakasonda, Philipo Bura, Seleman Jongo, Marry Mavula na Cosmas Chidumule.

Uongozi pia uliunda Kamati ya Kudumu ya Hamasa yenye watu 21 chini ya mwenyekiti Suma Mwaikenda na wajumbe wakiwa ni Saidi Mrisho, Clifford Lugora, Abdulmalik Hassan, Dominick Salamba, Hassan Bumbuli, Khamis Dakota, Leavan Maro, Dk David Luhoga na Jimmy Msindo.

Wengine ni Jimmy Mafufu, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya, Injinia Deo Mutta, Junior Ahmed, King Mwalubadu, Madaraka Malumbo, Haji Mboto na Miriam Odemba na Flora Mvungi.

Septemba 24, Mwenyekiti wa Yanga Dk Msolla kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji waliteua wajumbe 12 kuunda kamati ya mpya ya Ufundi ikiwa chini ya Salim Rupia akisaidiana na Dominick Albinus na wajumbe wakiwa ni Charles Mkwasa, Dk Jonas Tiboroha, Idd Kipingu, Kenny Mwaisabula, Said Maulid, Ally Msigwa, Sunday Manara, Ally Mayay, Saikolojo Chambua na Abeid Mziba.

Oktoba Mosi, Kamati ya Utendaji iliwachagua wajumbe 18 kuunda Kamati Mpya ya Ujenzi na Miundombinu ambayo iko chini ya Bahati Mwaseba na Athuman Kihamia.

Wajumbe ni Said Mrisho, Heliheli Muhulo, Isaac Usaka, Jumanne Werema, Abdallah Mrindoko, Buluba Mabelele, Gervas Kondombole, Hamad Islam, Ashura Ande, James Lobikoki, Peter Simon, Isaac Chanji, Said Hersi, Fundi, Fundi Sayore, Josephat, Peter, Baraka Igangula, Suma Mwaitenda na Madaraka Marumbo.

MSIKIE BUMBULI

Hata hivyo, Bumburi alipoulizwa juu ya utiriri wa kamati ndani ya Yanga alidai kuwa timu zote zimekuwa na kamati za namna hiyo, ila hawaziweki wazi kama Yanga inavyofanya mambo yake kwa uwazi ili kusaidia wanachama wake kujua vitu vinavyoendelea kwenye timu yao.

“Kila kamati ina majukumu yake, hakuna kamati itakayoingiliwa mfano Kamati ya Ujenzi inashauri mambo ya ujenzi kwa sababu ina wataalamu wa mambo hayo na inakuwa ikishauri Yanga namna ya kupata wakandarasi na baada ya hapo kuna Kamati ya Sheria ambayo nayo itakuwa inaangalia mikataba ya kisheria katika mikataba,” alisema.

“Kamati ya Ufundi inasaidia kushauri Kamati ya Usajili mambo mbalimbali, hivyo kamati hizi zinasaidia timu kuwa na mfumo mzuri ambao kila mmoja anakuwa akiwajibika kwenye nafasi yake kwa muda sahihi kuliko kila kitu kuiachia sekretarieti ifanye kazi yenyewe maana haitakuwa vizuri na vitu vinaweza vikakwama.”

KIPINGU ANENA

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu alisema uwepo wa kamati nyingi kwenye taasisi unapunguza majukumu kwa kamati kuu kutokana na mgawanyiko wa watu mbalimbali.

“Kitu cha msingi kinachopaswa kufanyika ni kuhakikisha kila kamati haivuki mipaka yake na kuepusha mgongano wa kamati nyingine, hii inamfanya katibu mkuu kuwa na kazi nyepesi ya kuzisimamia na kuweza kila jambo kufanyika kwa muda sahihi,” alisema Kipingu.

Aliongeza kuwa hata aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga alifanikiwa kwenye utawala wake kwa sababu aliweka kamati nyingi baada ya kuona Fifa (shirikisho la soka duniani) inavyofanya na hatimaye alifanikiwa kuwa na uongozi bora ndio maana hadi leo anakumbukwa kutokana na usimamizi wake uliokuwa mzuri.”