Yanga imeuficha ubingwa hapa

Muktasari:

Yanga inayonolewa na Mwinyi Zahera ndio imeweka makazi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa haijapoteza hata mchezo mpaka sasa, ikiwa imecheza mechi 19 na kukusanya alama 53 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 41 kwenye mechi 18,

SAWA Simba inaendelea kuwasha moto kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya makundi na jambo la kufurahisha zaidi ipo kileleni kwenye msimamo wa Kundi D, lakini hilo kamwe halijawafanya Yanga kuwa wanyonge.

Kwa sasa Yanga hawapo kwenye michuano ya kimataifa huku watani zao wakipanda ndege na kushuka kwenda kuwakilisha nchini, lakini shughuli inayofanywa na mabingwa hawa wa kihistoria kwenye Ligi Kuu Bara, imewafanya mashabiki wake kutembea kifua mbele na kuvaa zile jezi za Njano na Kijani muda wowote.

Yanga inayonolewa na Mwinyi Zahera ndio imeweka makazi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa haijapoteza hata mchezo mpaka sasa, ikiwa imecheza mechi 19 na kukusanya alama 53 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 41 kwenye mechi 18, KMC yenye alama 34 na mechi zake 22 kisha na Simba iliyocheza mechi 14 ikiwa na pointi 33.

Lakini, Yanga ambayo kesho Jumapili itashuka uwanjani kukipiga na Stand United pale mjini Shinyanga, imepewa tahadhari ya kuruka vigingi kadhaa ili iweze kutimiza malengo yake msimu huu.

Wachambuzi wa soka wanaamini Yanga ikifanikiwa kuruka viunzi hivyo hasa kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara basi Simba na Azam ambazo zinaifukuzia zitabaki kusoma ramani tu katika harakati za kubeba ubingwa.

Staa wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesema mechi za ugenini ndio kikwazo kikubwa kwa Yanga huku akizitaja timu za Biashara ya Mara ya Amri Said, ambayo ilianza vibaya lakini sasa imeimarika na kuanza kupata ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani.

“Kucheza ugenini ni changamoto kubwa, huko unakutana na timu ambazo zinapambana kujinasua kushuka daraja, viwanja sio vizuri hivyo wenyewe wanakuwa na faida kuliko mgeni. Hapa ndio naona kunaweza kuikwamisha Yanga, lakini ikifanikiwa kupenya basi kila kitu shwari,” alisema Lunyamila.

Hata hivyo, alisema kikubwa ambacho kinampa faida Zahera ni kuwafanya wachezaji wote ndani ya kikosi chake kuwa sawa kwa maana hakuna staa wa timu, jambo linalowapa ari ya kupambana uwanjani.

“Ameifanya Yanga kuwa moja kuanzia nje ya uwanja hadi uwanjani, hajaruhusu kuwepo mastaa wa timu, kitu ambacho kingesumbua kutokana na ukata uliopo kwa sasa,” alisema.

Naye mchambuzi mahiri wa Mwanaspoti, Ally Mayay alisema Simba na Azam hazina nguvu za kuizuia Yanga kuchukua ubingwa, lakini Yanga wanatakiwa kuwa waangalifu na timu za mikoani alizodai zinaweza kuikwamisha.

“Mechi ambazo Simba na Azam wamechemka ndizo ambazo Yanga wanatakiwa kushinda, mfano Simba ilipigwa na Mbao, Azam wametoka sare na Ruvu, hizo wahakikishe wao wanapata matokeo.

“Ikitokea wakikutana na hizo timu ambazo wanawania ubingwa pamoja, wanatafuta sare bado Yanga haitakuwa na hasara kwani, wana alama nyingi tayari kibindoni,” alisema.

Mbali na kutaja namna Yanga wanavyotakiwa kufanya ili waweze kupeleka ndoo Jangwani, alisema kuna wachezaji ambao ni injini ya timu kama Ibrahim Ajib, Paul Godfrey, Shaibu Abdallah ‘Ninja’, Kelvin Yondan na Fei Toto aliodai wametumika katika mechi nyingi