Yanga ilivyotema Makocha 12 ikisaka ubingwa

Kuna msemo wa kiandamizi kwenye ulimwengu wa idara ya ufundi kwenye soka kwamba makocha huajiriwa ili wafukuzwe.

Huu ni msemo maarufu duniani kote kwa sababu matokeo yanapoenda vibaya tu, mtu wa kwanza kutupiwa jicho huwa ni kocha, na kinachofuata baada ya jicho ni kutupiwa virago.

Lakini kwa Tanzania kufukuza makocha hakutokani tu na matokeo mabaya, bali ni fasheni.

Imekuwa fahari vilabu, hasa vikubwa, vya Tanzania kufukuza makocha hata wanapopata matokeo mazuri.

Hivi karibuni, klabu ya Yanga imemtimua kocha wake, Zlatko Krmpotic kutoka Serbia kwa kushindwa kwake kuifanya Yanga ifurahishe machi ya mashabiki wao.

Krmpotic anakuwa kocha wa 12 kwa Yanga tangu 2012 na kuifanya klabu hiyo iwe imetimua makocha wengi kuliko mataji ambayo imepata katika kipindi hicho.

Ukurasa huu unakuletea makocha wote 12 waliotimuliwa na Yanga tangu 2010.

Kostadin Papic (2010) -  Serbia

Alijiunga na Yanga mwaka 2008 akichukua mikoba ya Dusan Kondic. Alijiuzulu 2011 akipinga kitendo cha uongozi wa Yanga chini ya mwenyekiti Imani Madega kumteua Fred Felix Minziro kuwa kocha msaidizi bila yeye kushirikishwa.

 Sam Timbe (2011) -  Uganda

Alijiunga na Yanga 2011 kuchukua nafasi ya Papic na akaiwezesha kushinda ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Kagame, mara zote kwa kuipiku Simba. 

Kwa mataji hayo mawili, Timbe alibatizwa jina la kocha wa mataji lakini alifukuzwa miezi minane baadaye kufuatia matokeo mabaya.

Kostadin Papic (2011) -  Serbia

Kuondoka kwa Timbe kukamrejesha Paic Jangwani, kuendelea kukinoa kikosi cha wananchi.

Hata hivyo, ukazuka mgogoro mkubwa wa kiuongozi ulioanza kwa kujiuzulu kwa makamu mwenyekiti Davies Mosha.

Kilele cha mgogoro huo ni kichapo cha 5-0 kutoka Simba na mwisho wa msimu Yanga nafasi ya 3. Papic akafukuzwa.

Tom Saintfiet (2012) -  Ubelgiji

Kuondoka kwa Papic kukatoa nafasi kwa Tom Saintfiet aliyefahamika zaidi kama mtakatifu Tom.

Mechi ya kwanza alishuhudia kichapo cha 2-0 kutoka kwa Atletico Olympic ya Burundi kwenye Kombe la Kagame.

Timu hiyo ilikuwa ikifundishwa na Cedrik Kaze, ambaye alikaribia kutua kutua Yanga kabla ya Krmpotic, na sasa anatajwa tena kwamba huenda akakamilisha dili.

Saintfiet akaiongoza Yanga kushinda Kombe la Kagame lakini sare ya 0-0 na Tanzania Prisons kule Mbeya na kipigo cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, kikamgombanisha na bosi wake Yusuph Manji kiasi cha kutishiana bastola, na hatimaye akafukuzwa.

 Ernie Brandts ( 2012-13) -  Uholanzi

Shujaa wa Uholanzi wa Kombe la Dunia 1978, Ernie Brandts, akafuatia kubeba kikombe cha machungu cha Jangwani.

Akaanza kwa kichapo kutoka kwa Kagera Sugar lakini gari likawaka hadi akachukua ubingwa wa ligi kuu 2012/13.

Sare ya 3-3 dhidi ya Simba, timu take ikiruhusu uongozi wa 3-0 hadi mapumziko, kupotea ilimtia doa na safari yake ikakamilika kufuatia kichapo cha 3-1 kutoka Simba kwenye mechi ya bonanza la Mtani Jembe.

Hans Van Pluijm ( 2014) - Uholanzi

Alianza kazi Januari 2014 akiipokea timu iliyokuwa ikiongoza ligi kwa alama moja juu ya Azam FC.

Lakini kibao mwisho wa msimu Yanga ikaukosa ubingwa kwa Azam FC na mwenyekiti Manji hakufurahishwa.

Japo mambo yalifichwa kisiasa, lakini Hans alinitimuliwa, yeye na msaidizi wake Mkwasa, na kukimbilia uarabuni.

Marcio Maximo (2014) - Brazil

Kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars alishatajwa kujiunga na Yanga tangu 2012 kabla ya kiza kinene kutanda na msala kumuangukia mtangazaji na mchambuzi wa Clouds FM, Shaffih Dauda kwamba alimtisha kocha huyo eti Yanga hakukuwa salama kwake.

Safari hii akaja kuchukua mikoba ha Hans na akaanza vibaya kwa kuogopa kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame nchini Rwanda.

Maximo alitaka kupeleka kikosi cha vijana lakini CECAFA wakasema hayo ji mashindano ya wakubwa (senior teams).

Ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC kwenye Ngao ya Jamii ulionekana mwanzo mzuri kwake lakini ilipoanza ligi hali ilikuwa mbaya.

Alianza kwa kichapo cha 1-0 kutoka Mtibwa Sugar na safari yake ikahitimishwa na kichapo cha 2-0 mbele ya Simba kwenye Mtani Jembe.

Hans Van Pluijm ( 2015-16) -  Uholanzi

Hans van Pluijm akarejea Yanga na kuisaidia kushinda ngao ya jamii, ligi kuu na ubingwa wa kwanza wa mahindano mapya ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Pia aliiwezesha Yanga kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Hata hivyo, mwanzo wa kusua USA kwenye ligi ya 2016/17 kukamponza na kuondolewa kwenye nafasi yake.

Akageuzwa kuwa mkurugenzi wa ufundi na nafasi yake ya ukocha kuchukuliwa na George Lwandamina.

Mbinu kama hii Yanga waliitumia 2007 kwa Jack Lloyd Chamangwana (marehemu) ili ampishe kocha mpya Milutin Michu.

Hans akawa mkurugenzi wa ufundi kwa muda mfupi, halafu akaacha kazi yeye mwenyewe na kwenda kuwa kocha mkuu wa Singida United.

George Lwandamina (2016 - 2018) - Zambia

Akitoka kuiongoza Zesco kufika nusu fainali ya ligi ya Mabingwa Afrika, Lwandamina maarufu kama Chicken, aliisaidia Yanga kushinda ubingwa wa ligi kuu 2016/17 na kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Hata hivyo, kipindi chake kilikumbwa na ukata mkubwa kufuatia mwenyekiti Manji kujiuzulu na hela zake.

Lwandamina maisha yakamshinda, akabwaga manyanga 2018

Mwinyi Zahara (2018 - 2020) - DRC

Nafasi ya Lwandamina ikajazwa na Mwinyi Zahera.

Kocha huyu mwenye maneno mengi, akaisaidia Yanga nafasi ya pili kwemye ligi katika moja ya misimu mibaya zaidi kiuchumi klabuni hapo.

Kwa nafasi hiyo, Zahera alionekana shujaa lakini neema ilipokuja msimu uliofuata, matokeo hayakupatikana na uongozi wa Dkt. Mshindo Msolla ukamtimulia mbali.

Luc Eymel (2020) - Ubelgiji

Nafasi ya Zahera Zahera kwa muda na Charles Boniface Mkwasa na baadaye akaja mbelishi Luc Eymel.

Alianza kwa kichapo cha 3-0 nyumbani kutoka kwa Kagera Sugar.

Kichapo cha 4-1 kutoka Yanga kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports na matokeo ya kusuasua kwenye mechi za mwisho mwisho za msimu uliopita, vilimtia mhemko uliomsababishia kutoa kauli zilizotafsiriwa kuwa ni za kibaguzi, akaliwa kichwa.

Zlatko Krmpotic (2020) -  Serbia

Ndipo akatajwa Zlatko Krmpotic kuliongoza bench la ufundi la Yanga kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa VPL.

 Ujio wake wa kuchelewa ulisababisha timu kuanza kwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons kabla ya ushindi mfululizo hadi anafukuzwa.

 Sababu za kufukuzwa kwake ni aina mbaya ya mpira ambao Yanga inacheza chini yake.