Yanga ilipolala na viatu CCM Kirumba

Muktasari:

Katika mchezo uliopita wa ligi uliopigwa kwenye uwanja huo Jumatatu ya wiki hii, ambao Yanga walicheza na African Lyon, wadau wa soka waliondoka uwanjani hapo wakiwa wanasonya kutokana na kandanda bovu lililochezwa huku mpira ukipigwa upande mmoja.

MWANZA. ILIKUWA bonge la mechi unaambiwa, Kagera Sugar dhidi ya Yanga na mashabiki wa soka waliofika kuushuhudia mpambano huo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba waliondoka wakiwa na tabasamu baada ya kupata burudani tamu.

Katika mchezo uliopita wa ligi uliopigwa kwenye uwanja huo Jumatatu ya wiki hii, ambao Yanga walicheza na African Lyon, wadau wa soka waliondoka uwanjani hapo wakiwa wanasonya kutokana na kandanda bovu lililochezwa huku mpira ukipigwa upande mmoja.

Mpambano wa juzi Alhamisi licha ya Yanga kushinda mabao 3-2, ulikuwa na mvuto wa kipekee kwani ilipigwa kandanda safi lililofanya kila mtu aliyekuwapo uwanjani hapo kuondoka huku akiwa anatingisha kichwa kukubali kuwa mshindi alipatikana kwa pinde.

Inawezekana ulikuwapo uwanjani au uliangalia mpambano hili kupitia kwenye runinga, lakini hukuweza kuona matukio mbalimbali yaliyojiri uwanjani hapo, Mwanaspoti linakuletea mambo mbalimbali yaliyotokea kwenye mchezo huo.

Kagera kama Yanga

Yanga katika mechi zote walizocheza kwenye Uwanja wa Kirumba wamekuwa wakiingia na staili ya kipekee ambapo wamekuwa wakipita katikati ya mstari wa uwanja na kwenda moja kwa moja vyumbani.

Juzi Kagera Sugar nao waliingia na staili hiyo kwani walienda kuliegesha basi lao katikati ya uwanja na kupita kwenye mstari huo na kwenda moja kwa moja vyumbani.

Hata hivyo, wakati wakifanya hivyo mashabiki wa Yanga walianza kuwazomea wachezaji hao na benchi nzima la ufundi ambao walikuwa hawana muda nao.

Kadi ya nyekundu gumzo

Mwamuzi Alfred Vitalis kutoka Kilimanjaro juzi alizua gumzo kwenye mchezo huo baada ya kutoa kadi nyekundu kwa kipa wa Kagera Sugar, Jeremiah Kisubi kisha kuirejesha mfukoni na kutoa kadi ya njano.

Tukio lilitokea baada ya kipa huyo kuupangua kwa mkono mpira nje ya eneo lake jambo ambalo lilimfanya mwamuzi huyo kumwadhibu.

Kagera Sugar walinoga

Kila mtu aliyetoka uwanjani kwenye mchezo huo hata mashabiki wa Yanga waliwasifia Kagera Sugar kwani waliupiga mpira mwingi licha ya kupoteza mchezo huo.

Katika mchezo huo tangu unaanza wachezaji wa Yanga haswa mabeki walipata kazi ya ziada kuokoa mashambulizi langoni mwao.

Mashabiki Yanga noma

Mashabiki wa Yanga jijini hapa wamekuwa kivutio kikubwa kutokana na staili yao ya kipekee ya ushangiliaji kwenye uwanja huo wakati timu yao inapocheza.

Wakati mpira unaendelea mashabiki hao wanaokaa jukwaa la mzunguko upande wa kusini mwa uwanja wamekuwa kivutio kutokana na staili yao ya ushangiliaji ambapo wanatoka sehemu moja na kwenda nyingine huku wakiyakata mauno.

Mashabiki hao waliokuwa na matarumbeta wamekuwa wakitoka eneo lao na kwenda kwa wenzao ambao wapo jukwaa la upande wa kulia na kwenda kushangilia nao kwa kuserebuka kisha kurejea walipokaa.

Makambo Mwanza damudamu

Straika Heritier Makambo alifikisha bao lake la 15 la Ligi Kuu lakini mchezaji huyo amekuwa na upepo mzuri jijini Mwanza kwani katika mechi tano walizocheza Yanga msimu huu amefunga mabao matano.

Makambo alifunga bao katika mchezo wao dhidi ya Mbao akafunga tena katika mchezo wa FA dhidi ya Alliance kisha akapachika mawili kwenye mpambano wao dhidi ya African Lyon na juzi akatupia tena.

Ni mshambuliaji pekee wa Ligi Kuu aliyefunga mabao matano kwenye msimu mmoja katika uwanja wa Kirumba jijini hapa.

Bao la kideo

Kiungo Kassim Hamis alifunga bao tamu katika mchezo huo ambalo kipa wa Yanga, Klaus Kindoki, alijikuta akiutazama mpira ukitinga nyavuni.

Hamis alipokea pasi kutoka kwa Peter Mwalyanzi katika wingi ya kushoto kisha akasogea kidogo na kuachia shuti kali ambalo lilikwenda moja kwa moja kwenye nyavu ndogo kulia.

Bao hilo lilikuwa kama ni kufuta makosa yake kiungo huyo kwani tayari alikuwa amejifunga wakati wa harakati ya kuokoa mashambulizi langoni mwao.

Zahera afunguka

Mwinyi Zahera anasema mchezo ulikuwa mgumu kwao kutokana na uchovu wa wachezaji wake lakini anashukuru kwa ushindi huo.

“Niwapongeze wachezaji wangu mchezo ulikuwa mgumu kwetu, lakini walipambana na kupata ushindi,” alisema kocha huyo.

Nahodha huyu hapa

Nahodha msaidizi wa Kagera Sugar, Paul Ngalyoma alisema mchezo ulikuwa wa kwao kuweza kupata ushindi lakini hawakuwa na bahati na sasa wanakwenda kujipanga ili kumaliza vyema ligi hiyo na kukwepa janga la kushuka daraja.