Yanga haijabadili utamaduni, ni muda tu kwao

Dar es Saalam. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na mchambuzi, Ally Mayay amesema tatizo la Yanga ni muda tu kuwa na timu nzuri, akisisitiza utamaduni wa soka la Yanga la kutumia mawinga bado haujabadilika.

Yanga imekuwa na ushindi kiduchu katika mechi zake za Ligi Kuu licha ya kuwa nafasi ya tatu kwa pointi 10, sawa na Simba, wakati vinara wa Ligi Kuu, Azam FC wakiwa na pointi 12 kileleni.

“Ni mabadiliko tu ya makocha yameifanya kubadilika wakati mwingine kwa kutumia viungo wengi kuliko mawinga, hivyo kujikuta wakienda katika mfumo ambao unatumiwa zaidi na watani zao, Simba wa kucheza pasi fupi fupi.

“Hata hivyo kwa sasa kwa Yanga ilivyo kiwango si kipaumbele chao kikubwa zaidi ya ushindi kutokana na aina ya kikosi walichonacho, ambacho kina wageni wengi na hakina muunganiko, hivyo kujikuta wakipiga pasi ya kwanza ya pili wako golini,” alisema Mayay.

Mayay alisema hata kwa mawinga waliopo ndani ya kikosi hicho winga ambaye anaweza kucheza kuendana na asili ya soka la timu hiyo ni Mcongo Tuisila Kisinda kwani ana kasi kama ilivyokuwa kwa mawinga waliopita akiwemo Simon msuva.

Kiungo wa zamani wa timu hiyo, Sekilojo Chambua alisema hadi Yanga icheze soka la kueleweka ambalo mashabiki watalifurahia itachukua muda.

“Kila mtu anajua kuwa timu imebadilika sana, hivyo bado wachezaji hawajazoeana, itachukua muda kidogo. Hata hivi wanashinda, wanaendelea kujiamini zaidi,” alisema Chambua.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ’Jembe Ulaya’ alisema kulingana na aina ya wachezaji iliyonayo Yanga haiwezi kucheza aina ya soka walilocheza zamani.

“Enzi zetu ilikuwa tunacheza sana kwa staili ya mashambulizi ya kushtukiza yaani pasi ya kwanza ya pili tushafika golini lakini ilikuwa zamani.

“Mwambusi analijua soka la Tanzania, amsaidie Zlatko wakati huu wanapoipanga timu kuwa bora zaidi ya ilivyo,” alisema Malima.