Yanga akili zote kwa Township

Muktasari:

Kwa mujibu wa mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, kikosi hicho kinatarajiwa kuwasili saa 8 mchana tayari kwa kujiweka sawa na mchezo wao wa kesho dhidi ya Township.

KIKOSI cha timu ya Yanga kinatarajia kuwasili mchana wa leo Ijumaa kikitokea Visiwani Zanzibar ilikoenda kuweka kambi ya muda mfupi na kucheza mechi mbili za kirafiki, huku akili yao yote ikiwa ni kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana utakaochezwa kesho Jumamosi.
Mchezo huo wa raundi ya awali kwa mkondo wa kwanza utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa na Yanga ikiwa na kazi ya kulipa kisasi cha mwaka jana walipofungwa nyumbani mabao 2-1 na kwenda kuambulia suluhu ugenini na kutolewa kwenye raundi ya kwanza.
Kwa mujibu wa mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, kikosi hicho kinatarajiwa kuwasili saa 8 mchana tayari kwa kujiweka sawa na mchezo wao wa kesho dhidi ya Township.
Saleh alisema mechi mbili walizocheza dhidi ya Mlandege na kushinda mabao 4-1 kisha usiku wa jana kutoka sare ya 1-1 na Malindi, imepwa mwanga kulekea mchezo wa kesho ambao wamepania kupata ushindi ili kujiweka pazuri kwa mechi ya marudiano ugenini wiki mbili zijazo.
Mratibu huyo alisema wachezaji wana morali kubwa na wamejiweka fiti zaidi kupitia michezo hiyo ya kirafiki, huku wakiwa na mzuka wa kutaka kuwanyamazisha wapinzani wao wa CAF kabla ya kwenda kumalizana kwao.
"Kikosi kipo imara na kila mchezaji yupo katika hari nzuri ya mchezo ambao tunatarajia kuukamilisha nyumbani kwa kushinda idadi kubwa ya mabao bila kuruhusu nyavu zetu kutikiswa," anasema.
"Utakuwa mchezo wa kulipa kisasi baada ya klabu hiyo tunayotarajia kucheza nayo kutufunga na kutuondosha katika mashindano hapo awali," anasema Hafidh.