Yanga SC yapewa mbinu kuua Zesco

Muktasari:

Nyota hao waliotajwa na Mpepo ndio walioibeba Zesco kwa kufunga mabao kwenye michezo yote ya kuvuka hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako waliiondoa Green Mamba ya Eswatini kwa jumla ya mabao 3-0.

Dar es Salaam. Wakati straika David Molinga ‘Falcao’ jana aliendeleza makali yake jijini Mwanza akifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Toto Africans katika mechi ya kirafiki, Yanga wamepewa mchongo wa kuizima Zesco Jumamosi.

Yanga itaikabili Zesco kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi yao ya kwanza ya mtoano ya kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mshambuliaji wa Kitanzania, Eliuter Mpepo anayeichezea Buildcon FC ya Zambia, ameitaka Yanga kuwa makini na nyota wa Kenya, Jesse Were na Umar Kasumba, akisema ni wachezaji hatari kwenye safu ya ushambuliaji ya Zesco.

Mpepo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022, alisema ukiwaondoa washambuliaji hao, John Ching’andu naye anapaswa kutazamwa kwa sababu ni moja ya viungo wazuri kwenye kikosi hicho cha George Lwandamina.

“Nawajua vizuri Zesco kwa sababu kule Zambia tumekuwa tukitumia uwanja mmoja, kuna muda huwa tunasubiriana wakati wa mazoezi ili tupishane,“ alisema mshambuliaji huyo wa Kitanzania.

Akizungumzia udhaifu wao, Mpepo alisema upo kwenye eneo la ulinzi hasa kwa mabeki wanaocheza pembeni, Yanga wanaweza kujipatia mabao kupitia maeneo hayo kama watatengeneza presha ya mashambulizi.

Nyota hao waliotajwa na Mpepo ndio walioibeba Zesco kwa kufunga mabao kwenye michezo yote ya kuvuka hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako waliiondoa Green Mamba ya Eswatini kwa jumla ya mabao 3-0.

Straika wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ameishauri timu hiyo kujitahidi kutengeneza nafasi nyingi za kufunga tofauti na ilivyokuwa katika mechi za raundi ya awali dhidi ya Township Rollers ya Botswana ambapo nafasi za kufunga zilikuwa chache na walivuka kwa bao moja la frii-kiki na moja la penalti.

“Sio tatizo kwa timu kufunga mabao ya frii-kiki au penalti, lakini Yanga wasiyategemee sana kwani kuna timu nyingine ni nadra mabeki wake kutengeneza faulo au penalti, kama Yanga wakiyategemea maana yake ikitokea beki ya Zesco haitengenezi faulo au penalti, Yanga haifungi,” alisema Mziba.

Alishauri washambuliaji wa timu hiyo kuwa na kombinesheni bora ambayo itatengeneza mabao ya ‘muvu’ na ikitokea wamepata penalti au frii-kiki basi waitumie kuongeza mabao.

“Sina wasiwasi na beki ya Yanga, tatizo liko kwa washambuliaji, wapambane wapate mabao ya mipango iliyosukwa,” alisema.

Wakati Mziba akitoa ushauri huo, makocha wa soka nchini wamesema katika mchezo huo, Yanga itacheza dhidi ya timu bora yenye uwezo wa kumiliki mpira ambayo pia inawatumia mawinga wenye kasi kuamua matokeo.

Beki wa zamani wa Yanga na kocha wa Singida United, Fred Felix Minziro alisema kikubwa ambacho Yanga wanaweza kukifanya kuidhibiti Zesco ni kufunga magoli ya mapema.

“Wakifanya hivyo watawavuruga wapinzani wao, lakini wakiruhusu wao wafungwe mapema, mechi itakuwa ngumu kwao kwa kuwa Zesco ina uwezo mkubwa wa kumiliki mipira, watawachosha na mwisho watafungwa nyumbani,” alisema Minziro.

Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema, Zesco inacheza kwa kuwatumia mawinga wenye kasi, hivyo kuna haja ya walinzi wa Yanga kujipanga mapema kuwazuia viungo hao wasipenye kufanya mashambulizi

Hata hivyo, makocha hao wamesema Yanga bado kuna tatizo la kombinesheni ya timu hasa kuanzia katikati kwenda mbele, hivyo kuna haja pia ya kocha Mwinyi Zahera kufanyia kazi kasoro hiyo mapema.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ amesema Yanga inahitaji kufanya kazi ya ziada ili kuifunga Zesco.

“Wakiamua wanaweza, hata mchezo wa awali hakuna aliyetarajia wangeshinda Botswana,” alisema.

Molinga atisha

Straika Mcongo, Molinga jana alifunga magoli mawili na kutimiza mabao matatu katika mechi mbili za kirafiki mjini Mwanza.

Molinga alifunga mabao yote mawili kwa kichwa jana, huku la tatu likifungwa na iungo Abdulaziz Makame aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa kutokea nje kidogo ya boksi.

Jumapili, Molinga alifunga pia katika sare ya 1-1 dhidi ya Pamba FC.

Imeandikwa na Imani Makongoro, Eliya Solomon, James Mlaga, Mbushi Kwilasa na Saddam Sadick