Yanga Princess yapigwa nje ndani SWPL

Muktasari:

  • Naye kocha wa Simba Queens, Omary Mbweze alisema Yanga Princess anaamini msimu ujao itakuwa na ushindani kwa kuwa itakuwa imezoea ligi hiyo.

YANGA Princess inamaliza msimu vibaya baada ya kupigwa nje ndani na watani wao wa jadi Simba Queens kwenye ligi kuu ya wanawake Tanzania Bara (SWPL).

Mzunguko wa kwanza Yanga Princess iliambulia kichapo cha mabao 7-0, ikaonekana ni ugeni wa ligi hiyo, wadau wa soka wakiwapa nafasi ya kurudisha kisasi ya pili nayo wamepigwa mabao 5-1, hivyo wamesakamwa mara 12 langoni kwao.

Katibu Mkuu wa chama cha soka mkoa wa Dar es Salaamn (DRFA), Msanifu Kondo alitoa maoni kwa Simba Queens na Yanga Princess kwamba zinatakiwa kuwa na ushindani sawa kama ilivyo kwa timu za wanaume akiamini ndizo zinazoweza kuleta chachu ya maendeleo ya soka la wanawake.

“Afya ya Simba Queens ni Yanga Princess kufanya vyema, hapo ndipo ushindani utapatikana kwenye hizo timu kama ilivyo kwa wanaume ambao wakikutana nchi inatikisika, hivyo viongozi waweke mkazo kwa timu zao za wanawake”alisema.

Naye kocha wa Simba Queens, Omary Mbweze alisema Yanga Princess anaamini msimu ujao itakuwa na ushindani kwa kuwa itakuwa imezoea ligi hiyo.

“Wanacheza vizuri ila bado wanaonekana ni wageni na ligi, ndio maana tumeweza kuwafunga jumla ya mabao 12, wao wametufunga moja tu, tunahitaji ushindani kwenye soka la wanawake, wakajipange na sisi tutajipanga,” alisema.