Yanga Princess yakiona kwa Simba Queens

Muktasari:

  • Utani wa jadi hauishii kwenye timu za wanaume  za Simba na Yanga bali hata kwenye timu zao za wanawake, ndivyo ilivyokuwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam ambapo Simba Queens imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga Princess, hao mashabiki walivyokuwa wanashindana asikuambie mtu.

LEO ilikuwa mechi ya watani wa jadi kwa timu za wanawake kati ya Simba Queens na Yanga Princess, mchezo uliokusanya nyomi ya mashabiki ambao walikuwa wanaziunga mkono timu zao.
Simba Queens imeibuka kidedea kwenye mchezo huo baada ya kuwachapa watani wao Yanga Princess mabao 3-1, mchezo huo umepigwa Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo iliibua ushindani wa hali ya juu kwa mashabiki kutokana na jezi za timu zao, jambo lililofanya hata mechi kuwa na ushindani wa juu.
Mabao ya Simba Queens yamefungwa na Mwanahamisi Omary (bao moja) na Neema Kilinga mawili, huku watani wao Yanga likifungwa na Shelda Boniface.
Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' amesema ushindi huo walioupata kwa watani wao wa jadi, unawapa nguvu ya kujiamini kwenye mechi zilizopo mbele yao.
"Msimu huu kwetu tunapambana kadri tunavyoweza kuhakikisha tunanyakua taji la ligi kuu ya wanawake baada ya kwenda JKT Queens mara mbili mfululizo na mara moja kwa Mlandizi Queens tangu ianzishwe 2017 chini ya aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi,"amesema.