Yanga Princess yaapa kuivuruga Simba Queen

Muktasari:

  • Yanga Princess inaikabili Simba Queens ikikumbuka kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza kwa kupigwa mabao 7-0.

MWANZA. ACHANA na matokeo ya jana Jumatano  ya kulala kwa kichapo cha mabao 2-1 kwa Alliance Girls, timu ya Yanga Princess imesema kwa sasa inahitaji kulipa kisasi na kuweka heshima katika mchezo wao ujao dhidi ya Simba Queens.

Yanga Princess ambayo imekusanya pointi 19 na kukaa nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake,inatarajia kuwavaa wapinzani wao Simba Queens Aprili 22 mwaka huu.

Hata hivyo timu hiyo inawakabili wapinzani hao ikikumbuka kisago kikali cha mabao 7-0 walichopata katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza,hivyo kufanya mpambano huo kuwa mkali zaidi.

Kocha Mkuu wa timu hiyo,Mohamed Hussein alisema hatokubali tena kupoteza mchezo wao na watani hao na kwamba mapungufu yaliyoonekana kwenye mechi zilizopita atayafanyia kazi.

Alisema makosa ya Straika na mabeki wake kuruhusu na kukosa mabao mepesi atahakikisha anawaweka sawa ili watakapokutana na Simba Queens waweze kufanya kweli.

“Ni mechi ambayo tunaifikiria sana kuhakikisha tunashinda na kuweka heshima,tunakumbuka vizuri kupoteza mchezo uliopita kwahiyo hatutarajii kurudia tena makosa”alisema Hussein.

Kocha huyo ambaye aliwahi kukipiga Yanga,aliongeza kuwa anahitaji kumaliza Ligi wakiwa nafasi nzuri licha ya kwamba ishu ya Ubingwa imeshakuwa ngumu kutokana kushindwa kujinadaa mapema.

Husein alishauri Bodi ya Ligi nchini (TPLB) kuhakikisha wanafuatilia michezo iliyobaki kwani baadhi ya waamuzi wamekuwa wakishindwa kutumia sheria za soka katika mechi.

“Unakuta mwamuzi kwa kudhamiria anafanya maamuzi anayotaka mwenyewe,kwahiyo timu zinakata tamaa bora bodi ya Ligi ifuatilie kwa umakini,” alisema kocha huyo.