Yanga,Azam ziliyoacha rekodi kanda ya ziwa

Muktasari:

  • Makala hii inakuletea jinsi timu hizo zilivyoonyesha ubora na utofauti katika michezo yake ya Kanda ya Ziwa pamoja maisha waliyoishi jijini Mwanza.

MWANZA.TIMU za Yanga na Azam zimeacha historia kwenye Ukanda wa Ziwa baada ya kucheza mechi zote bila kupoteza na kuzifanya timu pinzani kubaki na maumivu kwenye Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.

Ndiyo. Klabu hizi kubwa zimeacha rekodi nzuri kwa jinsi zilivyoonyesha uwezo kuanzia maisha waliyoishi mikoani, ubora wa vikosi na nguvu ya mashabiki kuelekea mechi zao zote walizocheza huku.

Ikumbukwe, baada ya kufungwa kwa Uwanja wa Taifa na Azam Complex, timu hizo ziliamua kuweka kambi yake Mwanza, ambako kwa jumla hesabu zilikubali na sasa klabu hizo zinachekelea.

Makala hii inakuletea jinsi timu hizo zilivyoonyesha ubora na utofauti katika michezo yake ya Kanda ya Ziwa pamoja maisha waliyoishi jijini Mwanza.

Matokeo uwanjani

Hapa kila timu ilifanya kweli, lakini Yanga walitisha zaidi ya Azam kwa kushinda mechi zote nne mfululizo bila hata sare, tofauti na ‘Wanalambalamba’ waliotoa sare dhidi ya Mbao FC.

Azam walianzia mkoani Kagera katika mechi ya Kombe la Shirikisho kwa kuidunda Kagera Sugar bao 1-0 na kufuzu hatua ya nusu-fainali ya michuano hiyo.

Kama haitoshi timu hiyo tajiri, ilifanya kweli kwa kuifunga tena Kagera Sugar 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye dimba la Nyamagana jijini Mwanza.

Kwa upande wa Yanga wao walitisha kwa kushinda mechi nne ikiwa ni dhidi ya Alliance (FA na Ligi Kuu), African Lyon waliyowapiga 2-0 kabla ya kuwabwagaa Kagera Sugar 3-2.

Ushindi kwa Yanga ulikuwa ni rekodi ya kwanza kwa Kocha wake, Mwinyi Zahera ambaye ameonyesha ubora wake baada ya timu hiyo kusota kwa misimu miwili mfululizo bila kupata hata sare kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Matokeo mazuri kwa timu hizo yaliziachia ‘msala’ timu pinzani kutokana na vita ya kukwepa kushuka daraja inayowakabili Mbao, Kagera Sugar, Alliance na African Lyon, ambazo zote zipo katika nafasi mbaya.

Nguvu ya mashabiki

Yanga kwa kipindi ambacho imekaa Mwanza kujiwinda na mechi zake imekuwa ikitembea kifua mbele kutokana na sapoti ya mashabiki wake tangu wanatua kwenye Uwanja wa Ndege hadi uwanjani.

Ilishuhudiwa wanachama na wapambe wa timu hiyo kila mmoja akitaka kuonyesha ushiriki wake juu ya timu hiyo, jambo ambalo liliwapa morali wachezaji kupambana na kupata matokeo mazuri.

Zile huduma ndogo ndogo ikiwa ni maji mazoezi, usalama wa timu, usafiri wa kutoka kambini hadi uwanjani na mambo mengine vyote vilikuwa chini mashabiki wake.

Hali hiyo iliwafanya mabingwa hao wa zamani kutembea kifua mbele na hata ushindi kwenye mechi zote ulichangiwa na nguvu ya mashabiki ambao kila muda walikuwa wakijadili kupata pointi tatu kila mchezo kwenye dimba la Kirumba.

Maisha nje ya uwanja

Ukiachana na matokeo mazuri waliyopata Yanga, timu hiyo iliendelea kuwa juu kutokana na maisha waliyoishi kwenye hoteli ya kifahari ya JB Belmonte.

Pamoja na kwamba Azam nao walikuwa kwenye hotel nzuri, lakini gharama zao zilikuwa hazifui dafu kwa Yanga.

Iko hivi, Yanga walifikia Hotel ya JB Belmonte ambayo ipo katikati ya jiji, Barabara ya Kenyatta, huku Azam wao wakijichimbia katika hoteli ya Royal pembeni kidogo.

Gharama za hoteli waliyofikia Yanga chumba kimoja inaanzia Sh.70,000 hadi Sh.120,000 wakati Royal chumba kimoja kinagharimu kuanzia Sh. 60,000 hadi Sh.80,000 huku huduma ya chakula inajitegemea kwa hoteli hizo.

Yanga na Kirumba safi

Kwa mara ya kwanza timu ya Yanga iliweka rekodi ambayo haitasahaulika kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Kwa misimu miwili mfululizo, Yanga iliyokuwa chini ya Kocha George Lwandamina ilikuwa haijaonja ushindi wala sare yoyote ilipocheza kwenye Uwanja huo.

Lakini msimu huu Kocha Zahera ameweza kuwapa mashabiki wao kitu kipya roho inataka na wataendelea kumkumbuka Mkongo huyo kwa kuwaondolea aibu hiyo.

Zahera alitisha pia pale alipoiongoza Yanga kutinga hatua ya nusu-fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuing’oa Alliance FC kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kindoki habari nyingine

Kipindi cha nyuma, Kipa wa Yanga, Klaus Kindoki, alikuwa hana raha klabuni hapo akituhumiwa kufungwa mabao mepesi na kumfanya hata kocha wake kutomuamini katika kumchezesha.

Lakini unaambiwa kipa huyo amekuwa ‘lulu’ ndani ya Yanga hivi sasa baada ya kuiwezesha timu hiyo kufuzu hatua ya nusu-fainali ya Kombe la FA kwa kuokoa penalti tatu.

Katika mechi nne alizocheza mfululizo kwenye Uwanja wa Kirumba, ameruhusu mabao matatu na kuiwezesha timu kukusanya pointi 12 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 74.

Makambo acha kabisa

Ukizungumzia mafanikio ya Yanga hivi sasa, lazima utamtaja straika Heritier Makambo.

Nyota huyo raia wa DR Congo amekuwa akiibeba timu yake msimu huu kwa kufunga mabao muhimu.

Makambo ambaye ameshafunga mabao 15 hadi sasa alionyesha uwezo wake kwa kila mchezo kufunga bao katika uwanja wa Kirumba na kuweka rekodi ya kipekee.

Nyota huyu alianza kufunga bao wakati Yanga ikiitandika Alliance 1-0 kwenye mechi ya FA, kisha akatupia mabao mawili dhidi ya African Lyon na kisha kupachika bao moja dhidi ya Kagera Sugar.

Kasi hiyo ilimfanya kumuacha mpinzani wake, Meddie Kagere wa Simba, ambaye walikuwa sambamba kwa idadi ya mabao (14) katika mbio za kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora baada ya yeye kufikisha mabao 15, moja tu nyuma ya kinara, Salim Aiyee wa Mwadui, mwenye mabao 16.