Yanga Arusha yaifungia safari Zesco kwa vipensi

Muktasari:

Lumato alisema kuwa Lengo kubwa la safari yao ni kutoa hamasa ya ushangiliaji na kuisapoti timu yao ili iweze kufuzu hatua hiyo kwa kuungana na wanachama na wapenzi wa mikoa mingine kuujaza uwanja wa Taifa.

Arusha. Wanachama na mashabiki wa Yanga mkoani Arusha wako katika mkakati kabambe ya kuratibu safari yao ya kuelekea mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa sapoti kwa Yanga inayotarajia kuvaana na timu ya Zesco Septemba 14 mwaka huu.

Akizungumzia safari yao, katibu mkuu wa matawi ya Yanga mkoani Arusha, Bahati Lumato alisema wamehamasishana katika mashina na matawi yote ambapo hadi sasa wameshatoa oda ya magari matatu itakayobeba wanachama zaidi ya 80 waliothibitisha hadi sasa kushiriki.

“Tulitoa gharama nafuu ya usafiri kutoka Arusha hadi Dar es Salaam ni shilingi 40,000 tu kwenda na kurudi ambapo wanachama zaidi ya 150 walionyesha nia ya kutaka kusafiri lakini hadi sasa waliolipa hiyo nauli kwa mweka hazina ni watu 80 hivyo kwa sasa hao ndio tuna uhakika nao wa kusafiri ingawa bado wanachama na wapenzi wanaendelea kulipa”

Lumato alisema kuwa Lengo kubwa la safari yao ni kutoa hamasa ya ushangiliaji na kuisapoti timu yao ili iweze kufuzu hatua hiyo kwa kuungana na wanachama na wapenzi wa mikoa mingine kuujaza uwanja wa Taifa.

“Lengo lingine ni kumuunga mkono kocha wetu mkuu Mwinyi Zahera ambae amekuwa msaada mkubwa kwa timu yetu, lakini hivi karibuni wamekuwa wakim’beza na mavazi yake ya kimichezo anayovaa hivyo sisi kama Arusha siku hiyo kila mtu amenunua vazi la pensi na atalitinga siku ya mech hiyo”

Alisema kuwa wanatarajia kuondoka usiku wa siku ya ijumaa kutoka Arusha ili kufika Jumamosi asubuhi uwanja wa Taifa na baada ya mechi watafunga safari ya kurudi usiku huo huo.

Akizungumzia mchezo huo katibu huyo amesema kuwa wanaujua ukali wa aliyekuwa kocha wao George Lwandamila anayekinoa kikosi hicho, pia uwezo mkubwa walionao timu ya Zesco katika kumiliki mpira hivyo wanaweza kupata ushindi endapo wakifanikiwa kupata mabao ya mapema ili kubaki wakiwazuia katika kipindi cha pili.