Yanga, Simba mtegoni Kombe la Azam

Muktasari:

  • Tangu lilipoanzishwa katika msimu wa 2015/2016, timu nne tofauti zimetwaa taji la Azam Sports Federation ambazo ni Yanga, Simba, Mtibwa na Azam FC.

Droo ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Azam Sports Federation Cup itafanyika leo jijini Dar es Salaam huku uwepo wa timu kongwe za Simba na Yanga zikiwa na uwezekano wa kukutana.
Timu hizo mbili ambazo zote zimewahi kuchukua taji hilo kwa nyakati tofauti, ni miongoni mwa nane ambazo zimetinga hatua hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), droo hiyo itafanyika katika makao makuu ya Azam TV, Tabata jijini kuanzia saa 5.00 asubuhi.
Ukiondoa Simba na Yanga timu nyingine sita ambazo zinafanya jumla ya timu nane zilizotinga hatua ya robo fainali ni Azam, Ndanda, Alliance, Kagera Sugar, Namungo na Sahare All Stars.
Bingwa wa mashindano hayo ndiye hupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mashindano hayo yalianzishwa katika msimu wa 2015/2016 ambapo hadi sasa, timu nne tofauti zimewahi kutwaa taji.
Yanga ndio walikuwa wa kwanza kulitwaa katika msimu wa 2015/2016 na msimu uliofuata taji hilo lilitua mikononi mwa Simba.
Waliofuatia walikuwa ni Mtibwa Sugar  na msimu uliopita lilibebwa na Azam FC