Yanga, Azam, Simba njiapanda mikataba ya wachezaji

Sunday April 5 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Yanga, Azam, Simba njiapanda, mikataba ya wachezaji

 

By Charles Abel

Dar es Salaam. Klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara zimepatwa na wasiwasi wa kuondokewa na wachezaji kabla ya Ligi Kuu kuendelea tena baada ya kusimamishwa kutokana na mikataba ya nyota kadhaa kuishia ukingoni mwezi Juni, mwaka huu.
Wasiwasi huo unafuatia uamuzi uliotangazwa hivi karibuni na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa kusogeza mbele muda wa ukomo wa msimu huu kutoka mwezi Mei hadi Juni 30, ikiwa hali ya maambukizi ya virusi vya corona iliyosababishwa kusimamishwa kwa ligi itaendelea.
Mikataba ya kundi kubwa la wachezaji hasa wale wanaochezea katika klabu ambazo si Simba, Yanga au Azam itakuwa imefikia kikomo jambo linaloziweka katika hofu kwamba huenda zikakutana na changamoto ya kumaliza ligi vikosi vyao vikiwa pungufu au vikakosa idadi ya wachezaji ambao wanatosha kikanuni kwa ajili ya mechi kuchezwa.
Utamaduni wa idadi kubwa ya klabu za soka nchini kutoa mikataba mifupi ya muda wa miezi sita au mwaka mmoja kwa wachezaji unaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuziweka matatani katika msimu huu ambao ligi italazimika kuchezwa kwa muda mrefu zaidi tofauti na matarajio ya wengi kutokana na janga hilo ambalo limetikisa dunia.
Hali hiyo imesababisha klabu mbalimbali kujipanga kuanza mchakato wa kufanya mazungumzo na wachezaji ambao ifikapo mwezi Juni mikataba yao itakuwa inamalizika, huku pia zikisubiri huruma na mwongozo wa TFF ikiwa wachezaji hao hawatakuwa tayari kuzitumikia.
"Mfano ligi ikianza Juni na ikatokea wapo wachezaji ambao mikataba yao itakuwa imeisha, basi watamalizia sisi tutakuwa tunawapa mshahara, hiyo ndio itakayokuwa gharama kubwa kwetu kwani bajeti itakuwa imeongezeka," alisema katibu mkuu wa Prisons, Ajabu Kifukwe.
"Kwa sababu hata wao wanajua kwamba ni janga la dunia,wameruhusiwa kwenda nyumbani ili kulinda afya zao bila shaka naamini watakuwa waelewa kwani hata wakikomaa kuondoka hata huko hawatacheza watasubiri ligi iishe. "Wachezaji wengi ni askari, raia wachache ndio mikataba baadhi itaishi Juni,ila tupo tayari kukabiliana na hilo na kila kitu litakwenda sawa."
Mtendaji mkuu wa KMC, Walter Harrison alisema changamoto ya uwepo wa wachezaji ambao mikataba inaelekea ukiongoni inatakiwa ishughulikiwe kwa njia za busara.
"Ukifuatilia kisheria za mkataba, itakuwa ni haki ya mchezaji kwani utakuwa umeshamalizika lakini ikija suala la kutazama jambo hili kiungwana naamini kuna kitu kinaweza kufanyika kwa wachezaji na klabu kwani tatizo hili (la corona) hakuna ambaye alipanga litokee, hivyo kunaweza kufanyika majadiliano,"  alisema Harrison.
"Mfano tunaona huko Ulaya baadhi ya wachezaji kama Willian wa Chelsea, mikataba yao inaelekea ukingoni lakini wameahidi kucheza hadi pale ligi itakapomalizika kwa vile wanafahamu fika kuwa jambo hili ni tatizo la dunia na liko nje ya mipaka ya kibinadamu, hivyo tunaweza kulifanya hapa ila kama yupo ambaye hataona haja ya kufanya uungwana, tutamruhusu aondoke hatuwezi kumlazimisha."
Katibu mkuu wa Ndanda FC, Seleman Kachele alisema wao ndio wanaweza kuathirika zaidi kwa vile kundi kubwa la wachezaji wao mikataba inaisha Juni.
"Kama asilimia 70 hivi ya wachezaji wetu mikataba yao itakuwa imemalizika, hivyo kabla ya kufanya mazungumzo na TFF tutakaa chini na wachezaji na kuwaelezea ili kuona kibinadamu tunafanyaje kwa sababu watakuwa na haki kwani mikataba yao haionyeshi kwamba ikitokea majanga kama haya nini kifanyike," alisema.
"Na hili ni fundisho kwa klabu na wachezaji. Ikishindikana ndipo tutajaribu kuzungumza na TFF ili kuona wanatusaidia vipi kwa sababu tunafahamu kuwa hata wao hawakupenda jambo kama hili kutokea na walipanga ligi imalizike Mei ili waweze kuendana na ratiba za mashindano ya kimataifa."
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema kuwa suala hilo litategemea majadiliano baina ya pande husika.
"Muhimu ni maelewano," alijibu Kidao kwa ufupi.

Advertisement