Yanga, Azam, KMC zapewa mchongo

Tuesday July 23 2019

 

By Olipa Assa

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya kutangazwa ratiba ya michuano ya kimataifa, wadau wa soka wametoa maoni tofauti kuhusu ushiriki wa timu za Tanzania Bara Simba, Yanga, Azam na KMC.

Juzi, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilitangaza ratiba ya mashindano ya kimataifa ambako Simba itacheza na UD Songo ya Msumbuji, Yanga dhidi ya Township Rollers ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Azam itacheza na Fasil Kenema ya Ethiopia wakati KMC itavaana na AS Kigali ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumzia ratiba hiyo, mchambuzi Ally Mayay alisema klabu hizo nne zinapaswa kufuatilia rekodi ya wapinzani wao ili kujipa nafasi nzuri ya kujiandaa.

“Waarabu wakicheza na timu zetu utaona kuna kasoro wameona wakija ugenini wanapambana kupata sare ambayo kwao ni sawa na ushindi.

“Yanga si mara ya kwanza kucheza na Township Rollers, hii ni nafasi yao kuwatuma watu kujua ubora wao ili washinde nyumbani,” alisema Mayay.

Advertisement

Kocha Kenny Mwaisabula alisema anaamini timu za Tanzania zinaweza kufika mbali endapo watatumia vyema mechi za nyumbani kupata ushindi.

Wakati Mwaisabula akishauri timu hizo kushinda nyumbani, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila jambo pekee linaloweza kuzivusha timu hizo ni nidhamu.

“Ni wakati wa Simba, Yanga na Azam kufanya kitu, zimekuwa zikipata nafasi ya kushiriki mara kwa mara michuano ya kimataifa, zitakuwa zimejifunza cha kufanya, lakini KMC ina changamoto kidogo”, alisema Katwila.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismaili Rage, alisema kila mchezaji wa timu nne anatakiwa kutafakari namna atakavyotoa mchango katika michuano ya kimaifa.

“Wachezaji akili zao zianze kufikiria ukubwa wa majukumu yaliopo mbele yao, hatua hiyo itawafanya wawe na juhudi binafsi uwanjani kwa kila mmoja kujituma,” alisema Rage.

Advertisement