JICHO LA MWEWE: Yanayompata Samatta, yamenikumbusha Madaraka Seleman

NAZIDI kupata hofu kuhusu Mbwana Samatta. Mtu mmoja ameninong’oneza Aston Villa imemwambia Samatta hayupo katika mipango yao. Napata hofu kweli kweli. Wakati mwingine lisemwalo lipo.

Majuzi nilikuwa naona uwezekano wa Samatta kubakia pale. Ghafla katika pambano la Kombe la Carabao dhidi ya Burton, Samatta alikaa nje. Alianza mshambuliaji mpya, Ollie Wilkins na baadaye akaingia straika mwingine wa Kiingereza, Kiernan Davis.

Kufikia hapo nilinyong’onyea kwa kujua kwamba huenda ni kweli Villa imedhamiria kuachana na Samatta. Nilidhani baada ya Ollie angeweza kuingia Samatta, lakini kocha anapoamua kukuondoa katika mipango yake hali inakuwa kama ilivyokuwa.

Kwanini Villa inataka kuachana na Samatta? Inawezekana wamejipa sababu kwamba ameshindwa kuingia katika soka la Kiingereza.

Amefunga mabao mawili tu katika mechi 16 alizocheza. Wanaweza kuhalalisha kwamba soka la Kiingereza limemshinda.

Kwa sasa Samatta ni mfungaji zaidi. Ameachana na ile tabia yake ya kuchukua watu kutoka mbali na kwenda kufunga. Wakati yupo Genk aliwahi kuniambia kocha wake alimtaka akae katika nafasi ya kufunga zaidi na asijihangaishe kwenda maeneo mengine ya uwanja.

Akiwa na Genk, Samatta alikuwa anaonekana anafunga mabao rahisi tofauti na klabu nyingine alizopitia. Wazungu wa kule walimjulia na wakawataka mastaa wenzake wamchezeshe katika eneo la mwisho. Na kwa sababu alikuwa staa wa timu ilikuwa rahisi kwa wenzake kumchezesha.

Pale Aston Villa staa wa timu ni kiungo mbinafsi, Jack Grealish. Mgumu kuuachia mpira kwa haraka. Anafanya anachojisikia lakini muda mwingi amejikuta akishindwa kuwachezesha washambuliaji wake zaidi ya yeye mwenyewe kujitafutia nafasi binafsi za kufunga. Haikushangaza alipoibuka kuwa mfungaji wao bora msimu uliopita.

Pale England wengi wanamsifu Davis kwa sababu anatumia sana nguvu. Inawezekana Waingereza wameona anafaa zaidi kuliko Samatta ingawa ni wazi kwamba katika suala la ufungaji bado hawezi kumfikia Samatta.

Villa hawajataka kutumia ubora wa Samatta na inawezekana wameamua kushughulika na mapungufu yake.

Kama timu ingekuwa inamfikia Samatta mara kwa mara nadhani angefunga zaidi. Lakini kumbe timu yao ni mbovu na inahitaji watu wanaosukumana zaidi. Labda kwa hapo Samatta hawezi kufaa.

Inawezekana ndio maana wanataka kumbakisha Davis na kumuondoa Samatta.

Samatta wa leo anajua kucheza na nafasi zake. Amejikita katika kufunga zaidi na sio kusukumana zaidi. Alipokuwa Genk alifunga mabao mengi kiasi cha Waingereza kumuona. Nashangaa kwanini Waingereza hawataki kumchezesha kwa namna ambavyo atafaa kuwasaidia.

Ni hapa ndipo nilipojikuta ghafla namkumbuka mtu aliyeitwa Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’. Staa wa zamani wa Simba, Majimaji na Taifa Stars. Huyu ungeweza kuwajumlisha Samatta na Davis kwa wakati mmoja.

Madaraka aliweza mapambano ya nguvu. Aliyapenda. Alikuwa kiboko ya mabeki katika suala la matumizi ya nguvu, lakini hapo hapo alikuwa na jicho la kuziona nyavu. Miaka 35 nyuma kama Waingereza wangeweza kutunyanyasa kwa sababu ya Samatta basi tungewapelekea Madaraka.

Madaraka angecheza mpira wa Kiingereza ambao wanautaka na wanaupenda. Angekuwa bora kuliko kina Emil Heskey ambao walikuwa na uwezo wa kusukumana tu bila ya maarifa. Madaraka angewapa mambo yote mawili.

Wakati mwingi tunakumbushwa tusiupende sana uzamani, lakini ukweli unabakia pale pale kwamba zamani tuliwahi kuwa na kizazi bora zaidi cha soka ambacho kilikuwa na mambo mengi uwanjani. Mchezaji mmoja anakupa nguvu, kasi, maarifa na ufundi wa kuziona nyavu.

Kama kina Madaraka wangecheza zama hizi nadhani tungekuwa na mastaa wengi wanaotamba Ulaya. Hata katika maeneo ya ulinzi tungekuwa na mastaa wengi wanaotamba katika nchi za nje pengine kuliko ilivyo sasa ambapo wachezaji wengi wa Kitanzania wanaotoka nje ni wale wanaocheza nafasi za mbele.

Hapa nchini hata ukitazama ni wazi kwamba mabeki wamekuwa wababe kuliko washambuliaji. Kina Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Paschal Wawa na wengineo wamekuwa wababe kwa washambuliaji tofauti na ilivyokuwa zamani.

Zamani mabeki walikuwa wakipata shida kutoka kwa washambuliaji wakorofi na wenye maumbo makubwa kama Madaraka. Hawa ndio wangeenda kuwezana na Waingereza kama wanavyotaka. Walikuwepo kina Edward Chumilla, Fumo Felician, Juma Mgunda na wengineo ambao wangeweza kucheza soka la Kiingereza katika misingi ambayo Waingereza wanaitaka.

Siku hizi kina John Bocco wanaonewa na mabeki. Muda mwingi wanaishia kulalamika kwa waamuzi wakati zamani kina Kitwana Manara ‘Popat’ walikuwa wanaongoza kwa kulalamikiwa na mabeki kwa kuruka na viwiko na kucheza faulo nyingi uwanjani.

Mshambuliaji wa mwisho katika zama za karibuni ambaye alikuwa ananifurahisha kwa kusumbuana na walinzi kwa matumizi ya nguvu na ubabe alikuwa Monja Liseki.

Vile ndivyo mshambuliaji anavyopaswa kuwa. Mshambuliaji lazima ahakikishe kwamba mabeki hawana raha hata kama asipofunga.