Wosia wa Mzee Majuto kwa watoto wake

Friday August 10 2018

 

By Rhobi Chacha

Donge, Tanga. Mtoto wa marehemu Amri Athumani ‘Mzee Majuto’, Hamza Athumani  amesema baba yao aliwaachia wasia watoto wake siku moja kabla ya kifo chake.

Hamza ambaye ni mtoto wa nne kati ya 10 wa Mzee Majuto alisema hayo leo alipopewa nafasi ya kutoa wasifu wa baba yake baada ya kisomo.

Julai 7, 2018 alienda Hospital ya Taifa ya Muhimbili akiwa na Rais wa Shirikisho la  filamu, Simon Mwakifamba walipofika Mzee Majuto akaanza kumwambia nyinyi ni  watoto wangu wote naomba mpendane, msibaguane, kielimu na kifedha.

Hamza alisema yeye anawaomba ndugu zake wafuate maneno ya baba yao aliyosema kabla ya kifo chake.

"Ndugu zangu…ndugu zangu, ndugu  zangu...nawaita mara tatu na nawaomba tufuate wosia wa baba aliotuachia, amesema tupendane tusaidiane na wote ni watoto wake" alisema Hamza

 Aidha Hamza aliwaomba tena ndugu zake kwa kuwasisitizia kuwa, wasifuate maneno ya nje na wasiwavuruge kwani kuna maneno yanazungumzwa kuhusu familia ya Mzee Majuto bila ya kuyajua kwa undani, hivyo wafahamu kuna watu wanashida na sio wao.

Hamza alisema Mzee Majuto ameacha watoto 10 na wenzao watano wamefariki. Pia, ameacha mke mmoja.

Hamza alitoa shukrani kwa watu waliokuwa bega kwa bega toka kuanza kuumwa kwa Mzee Majuto hadi kifo chake ambaponi Rais John Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Makamu wa Rais mama Samia Suluhu, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Said Salim Bakharesa pamoja na wasanii wote.

Advertisement