Winga Simba afunguka kuutosa ukocha

Muktasari:

Suluja ametamba kwenye soka la Tanzania akiwa na klabu ya Simba kwa sasa ni katibu wa chama cha soka wilaya ya Geita mjini.


Mwanza. WAKATI wachezaji wengi wa zamani kwa sasa wakiwa wamejiingiza kwenye ukocha hali imekuwa tofauti kwa winga Mnenge Suluja ambaye amekiri wazi kuwa hafikirii kabisa kujiingiza kwenye kazi hiyo kwani ni ngumu sana.

Winga huyo wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa ni Katibu wa Chama cha Soka wilaya ya Geita Mjini (Gerefa) amesema kufundisha soka kwenye klabu za Tanzania kunahitaji kujitoa sana.

Amesema wadau wengi wa soka wamekuwa wakimuliza kuhusu kuwa kocha kwenye timu mbalimbali na amewajibu kuwa hawezi kufanya kazi hiyo na sasa ataendelea kuwa mwanamichezo kwa njia nyingine lakini sio kufundisha kwenye timu mbalimbali.

“Sifikirii kabisa kufundisha soka kwenye klabu maana naona makocha wanavyopata tabu kwangu sitaki hili jambo lijitokeze ndio maana umeona sijakimbilia huko,”

“Kwa sasa nimesomea ukocha kozi ya awali lakini nina mpango wa kufika hadi kwenye leseni B lakini sitofundisha timu yoyote labda niwe nafundisha vijana kwenye vituo vya kukuzia vipaji lakini sio kwenye klabu,”amesema na kuongeza

“Kwangu siwezi kuvumilia kabisa manyanyaso. Ukiangalia makocha wengi wanabebeshwa sana mzigo wa lawama timu inapokuwa inafanya vibaya lakini unakuta kosa sio la kwake, mimi kwangu hapana,” amesema  Suluja.