Wimbo wa Serena Williams watikisa dunia

Muktasari:

Wimbo wa Serena Williams 'I Touch Myself' umeteuliwa kuwa wimbo bora kati ya zilizotungwa kwa ajili ya maadhimisho ya mwezi wa kupiga vita ugonjwa wa kansa ya matiti.

Los Angeles, Marekani. Wimbo uliowekwa juzi jioni kwenye mtandao wa Instagram na mcheza tenisi mahiri wa Marekani, Serena Williams uitwao 'I Touch Myself' ndio uliotingisha kwa kusikilizwa zaidi na watazamaji.

Serena bingwa mara 23 wa mataji makubwa duniani ya tenisi ya Grand Slam, aliutupia wimbo huo aliourekodi mwenyewe akisema ni maalumu kwa ajili ya kumkumbuka mwanamuziki na mwigizaji Chrissy Amphlett kutoka Australia.

Chrissy Amphlett alifariki Dunia, Aprili 21, 2013 kutokana na ugonjwa huo alibainika kuwa nao dakika ya mwisho ukiwa umeshamuathiri kwa kiasi kikubwa na hivyo kushindwa kutibiwa.

Serena alisema wimbo huo 'I Touch Myself' unawahimiza watu wote kuchukua hatua ili kupambana na ugonjwa huo ambao ni hatari na bado hauna dawa ya uhakika kwa wanaochelewa kubainika na pia hauna chanjo.

"Video hii ya wimbo wangu ‘I Touch Myself’ ni mradi uliobuniwa kwa ajili ya kuikumbusha na kuihamasisha jamii kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kansa ya matiti unaowakumba wanawake na leo nimeutoa maalumu kukumbukia kifo cha mwanamuziki na mwigizaji Chrissy Amphlett,” alisema Serena.