Wikiendi ya mabao 11 kwa mastaa wa wageni, tujipange

WIKIENDI nyingine ngumu kwa soka letu niliishuhudia majuzi. Hii hapa iliyopita. Wakubwa wa soka walikuwa katika viwanja vitatu tofauti na tulichoshuhudia ni mabao 11 kutoka kwa wachezaji wa kigeni, hasa washambuliaji.

Hapa Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam, Yanga walifunga mabao matatu ya ushindi dhidi ya Coastal Union. Wafungaji? Mawili kutoka kwa viungo wa kimataifa wa nchi mbili tofauti. Moja lilifungwa na kiungo wa Angola, Carlinhos, jingine likafungwa na kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima.

Bao la tatu lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Yacouba Sogne ambaye kama ilivyo kwa Carlinho naye alipokewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga waliojitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati wa usajili. Macho mengine yalikwenda Chamazi. Watoto wa Mzee Bakhresa, Azam FC walicheza na Kagera Sugar pale Mbagala. Azam waliondoka uwanjani na ushindi wa mabao manne. Mawili yalifungwa na staa wa Zimbabwe, Prince Dube, moja likafungwa na Mzambia Obrey Chirwa na jingine na staa wa Ivory Coast, Richard Djodi.

Kule Dodoma, makao makuu ya nchi wakati huu wabunge wakiwa hawapo eneo hilo huku wakiwa wametawanyika kutafuta nafasi za kurudi tena, Simba walipeleka kikosi chao kamili na kuiadhibu JKT Tanzania kwa mabao 4-0.

Nyota wa Rwanda, Meddie Kagere alifunga mabao mawili, staa wa Kicongo, Chris Mugalu akafunga moja, halafu Mmakonde kutoka Msumbiji, Luis Miquissone akafunga jingine. Hakukuwa na nafasi kwa Mtanzania kufunga bao.

Hapa ndipo tulipofikia. Ninawakumbusha tu wageni kufunga sana ni kwa sababu kuu ya kwamba wanapata zaidi nafasi ya kucheza katika vikosi vya timu za kwanza za klabu hizi kubwa tatu nchini.

Anayeweza kutuwakilisha kupambana nao ni John Bocco pekee. Alianza akiwa Azam na sasa yupo Simba. Huyu ndiye ambaye anaweza kuwekwa kapu moja na wageni hawa katika eneo la ushambuliaji. Nyakati za kina Mohamed Hussein zimeondoka.

Lakini hata majuzi kulikuwa na kina Saimon Msuva. Inaonekana wazi kwamba hata wao wameshindwa kutoa warithi wazuri kwa kina Juma Mahadhi na Miraji Athuman na wengineo ambao tulitazamia wachukue nafasi zao.

Halafu kuna nafasi nyingine uwanjani ambayo imetwaliwa na wageni. Tazama katika orodha hapo. Kuna wachezaji kama watatu hivi ambao ni viungo wachezeshaji na wamefunga. Carlinhos, Haruna na Miquissone. Inatupa ujumbe gani? Kwamba eneo hilo kwa sasa linatawaliwa na wageni zaidi.

Haikuwa wiki ya Clatous Chotta Chama au Tonombe Mukoko, lakini si ajabu nao ungesikia wamefunga. Zamani nafasi hizo zilikuwa zinachezwa na kina Charles Boniface Mkwassa, Hamis Gaga, Athuman China na wengineo. Walikuwa wanafunga kama hawa kina Miquissone.

Hii ina maana mbili. Kwanza nafasi hizo kwa sasa zimeangukia zaidi kwa wageni, lakini pili inaonekana wageni wenyewe wana maarifa makubwa ya kufunga na kutengeneza nafasi kuliko wazawa. Hata nje ya vikosi hivi vitatu kuna wachezaji wachache sana wanaoweza kupambana na hawa. Labda Luis Kikoti wa Namungo. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiwawalalamikia washambuliaji wetu. Kwa nini hawaonyeshi makali yao kama zamani? Huu ni ushahidi tosha. Kwanza kabisa wameshindwa kupata nafasi ya kuwepo katika vikosi vya kwanza vya timu hizi. Labda Bocco pekee.

Lakini pia inaonyesha kwamba sio kwa bahati mbaya kwamba wapo huko walipo. Hawa wageni wanaocheza Simba, Yanga na Azam wanajitahidi kuonyesha utofauti wao. Kwa sasa ndio wameshika roho ya hizi timu achilia mbali washambuliaji ambao wamekuwa wapachikaji wakubwa wa mabao.

Na katika eneo hili lazima tuambiane ukweli kwamba viungo wetu wanahitaji kubadilika. Kwa sasa inaonekana tuna viungo wengi ambao wanapiga pasi nyingi za pembeni kuliko za mbele. Wengi wajifunze kupitia viungo wa kigeni wa sasa ambao mawazo yao yapo mbele zaidi.

Kwa upande wa ushambuliaji sijui tutafanya nini zaidi lakini ukweli ni kwamba wengi wao wanatuangusha. Hatuzalishi tena washambuliaji wa viwango vya juu kama ilivyokuwa kwa kina Edward Chumilla, Mohamed Salim, Juma Mgunda, Mohamed Hussein na wengineo.

Majuzi niliwahi kuandika hapa kwamba kwa zamani hata timu za mikoani zilikuwa na washambuliaji hatari. Ukienda Mtwara unakumbana na Ildephone Amlima, ukienda Mbeya unakumbana na Jimmy Morred, ukienda Dodoma unakutana na Mohamed Mbuguni. Kokote unakokwenda unapewa tahadhari ya kukumbana na walau mshambuliaji mmoja hatari.

Kwa sasa nje ya Simba, Yanga na Azam tunapewa tahadhari ya kukutana na Reliants Lusajo wa KMC au Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar. Tazama pengo kati ya mfungaji bora, Meddie Kagere na wengineo. Unagundua ni pengo kubwa.

Kuna maeneo mawili katika soka letu yamepwaya zaidi ukilinganisha na zamani. Eneo la golikipa na ushambuliaji. Kuna mahala hapo tumekwama. Hatuzalishi wachezaji kama mastaa kama zamani. Maeneo mengine tunajaribu lakini maeneo hayo mawili ambayo ni muhimu tumekuwa tukizalisha wachezaji kwa kusuasua.

Hatujui kwa nini zamani tulikuwa tunapata washambuliaji hatari na walinzi wazuri. Wataalamu wanaweza kutuambia ni kitu gani kinatukwamisha kwa sasa lakini hatuwezi kuficha ukweli kwamba wageni wanatutawala kwa kiasi kikubwa.

Nilikuwa naushangaa mjadala uliokuwa unaendelea hivi karibuni kwamba tunapaswa kupunguza wachezaji wa kigeni kwa ajili ya kulinda wazawa wetu. Haukuwa mjadala wenyewe afya. Kinachoendelea kwa sasa kinadhihirisha kwamba tulikuwa tunataka kuwaonea wachezaji wa kigeni kwa gharama za kulinda watu wasio na uwezo.