TASWIRA YA MLANGABOY : Wiki ya Mwananchi, Simba Day ziwe kisasa zaidi

Saturday August 3 2019

 

By Andrew Kingamkono

MAISHA yanaenda kasi hakuna mfano kila mmoja anapambana na hali yake katika kuhakikisha mambo yanakuwa sawa.

Pamoja na ugumu huo, Tanzania sasa kumeibuka jambo ambalo ukiliangalia kwa jicho la kawaida unaweza kusema halikuhusu kwa sababu halijakupata.

Suala la utekaji wa watu pamoja na mauaji yanayoendelea kwa sasa nchini yatia doa kwa namna moja au nyingine. Unaweza kusema kwa nini leo Taswira imeamua kuzungumzia suala hili?

Ni kweli hapa tunajadili michezo, lakini itakuwa ni kujidanganya kwa kufanya hatuoni yanaotokea nchini kwa sababu tunazungumza michezo.

Naamini furaha ya kuwa uwanjani kushabikia mpira au mchezo wowote itakuwa vizuri tukiwa na uhakika ya kesho yetu.

Naamini serikali imeliona suala hili na sasa kwa kutumia vyombo vyake italifanyia kazi na kulimaliza mapema kwa ustawi wa Tanzania yetu.

Advertisement

Ukiacha suala hilo, Taswira inajua wiki hii mashabiki wa soka hasa wale wa Simba na Yanga watakuwa na wiki nzuri.

Agosti nne itakuwa ni Wiki ya Mwananchi, wakati Agosti 6 itakuwa ni Simba Day ni matamasha makubwa yanayoongeza hamasa kwa soka letu.

Ukiziangalia klabu hizo kongwe nchini Simba na Yanga zimefanya usajili wa kishindo na kambi zao Morogoro na Afrika Kusini zimeripotiwa kwa kishindo kikubwa.

Hakuna shabiki wa timu hizo mbili anayetaka kukusoa kushuhudia Wiki ya Mwananchi ili kuwaona nyota wao wapya kabla ya Simba Day nayo itakuwa na mambo kama hayo.

Klabu hizo zimeanza kwa kutembelea hospitali na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini katika kuelekea katika kile.

Taswari inaamini hii ni fursa kubwa kwa viongozi wa klabu hizi kutegeneza fedha za kuwasaidia kulipa mishahara ya wachezaji wao pamoja na kuziendeleza klabu hizo.

Naamini viongozi watatumia matamasha haya kuuza jezi kwa kiwango cha juu hasa kwa kuangalia wale wachezaji wao wapya ambao majina yao yameteka nchi kwa sasa.

Viongozi wa Simba na Yanga hawatakiwa kufanya kosa lilelile la kuacha wezi wachache wakatumia fursa hiyo kujitajilisha kwa kuuza jezi na kuziacha timu hizo zikiwa katika umasiki ule ule.

Tunahitaji kuona Wiki ya Mwananchi na Simba Day zikiwa siyo siku tu za kuwatambulisha wachezaji wapya, bali ziwe daraja kuwafanya mashabiki wa klabu hizi kununua jezi halisi kutoka kwa wauzaji wanaotambulika na klabu hizo.

Mbali ya jezi na vifaa mbalimbali vya michezo nadhani sasa wakati umefika kwa viongozi wa klabu hizo kutumia siku hizo kuuza vitabu na majarida yaonayoonyesha klabu hizo zimetoka wapi na zinaenda wapi.

Tanzania kumekuwa na tatizo la kuhifadhi kumbukumbu hasa takwimu za wachezaji waliopita na kutamba, nadhani wakati umefika sasa kwa vitengo vya habari vya klabu hizo kuwapa nafasi mashabiki kuzijua timu zao kwa kuweka kumbukumbu za wachezaji wao.

Naamini wakija uwanjani hawataona picha za wachezaji wa sasa tu, bali hata wale wa miaka sitini zile za rangi nyeupe na nyeusi zikiwa zimepamba uwanjani ili kuonyesha kweli ni tamasha la kubaki katika kumbukumbu ya mashabiki kwa muda mrefu.

Mechi zitakazochezwa haziwezi kuleta hamasa pekee, bali kwa matukio makubwa yatakayokuwa yakifanywa kuanza mwanzo hadi muda mchezo.

Naamini nitawaona wazee waasisi wa klabu hizi, viongozi waliopita pamoja na magwiji wa zamani waliotamba wakipita uwanjani hapo hapo ndiyo maana hali ya matamasha makubwa ya aina hii.

Jambo kubwa zaidi nataka kuzikumbusha klabu hizo pamoja na kufanana kwa Wiki ya Mwananchi na Simba Day ni aibu kwao kwa miaka zaidi ya 80 tangu kuanzishwa kwao hawana viwanja.

Tafuta picha tamasha la Wiki la Mwananchi lingefanyika kwenye Uwanja wa Kaunda au Simba Day inafanyika Bunju ni fahari gani mashabiki wa timu hizi wangejisikia, lakini wote wanalazimika kugombea Uwanja wa Taifa.

Naamini ajenda ya ujenzi wa viwanja inapaswa kuwa kauli mbiu kuelekea katika matamasha haya, haiwezekani Gwambina katimu kapya cha Mwanza kinamiliki uwanja, tena mzuri tu huku Simba na Yanga zikiwa hazina viwanja hata vya kuchukua mashabiki 20,000 tu.

Mwisho lakini si kwa umuhimu matokeo ya mechi za Wiki ya Mwananchi na Simba Day yasiwachanganye na kusahau kuwa kuna mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika zinakuja mbele.

Hakuna cha ziada zaidi ya mashabiki wa Yanga na Simba kujitokeza kwa wingi viwanjani na kuziunga mkono katika matamasha haya makubwa.

Mechi hizi ni muhimu kwa Simba na Yanga kufuzu ili kuzidi kujijengea heshima katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Simba ilifanya vizuri msimu ulioisha kwa kufika robo fainali, tunazitaka timu hizo pamoja na KMC na Azam FC kufanya vizuri zaidi msimu huu.

Advertisement