Wenger kupewa Qatar Kombe la Dunia 2022

Thursday January 10 2019

 

LONDON, ENGLAND.NI hivi Arsene Wenger anaweza kubamba dili jipya la kazi baada ya Qatar kumweka kwenye orodha ya kumtaka awe kocha wao mkuu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022.

Kocha huyo Mfaransa kwa sasa yupo tu akisubiri kazi mpya baada ya kupigwa chini na Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kudumu na timu hiyo kwa miaka 22.

Taarifa za kutoka Ufaransa zinadai wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia wanamtaka kocha huyo akanoe kikosi chao kutokana na uzoefu wake kwenye mchezo wa soka.

Huko nyuma, kabla ya kuibuka kwa dili hilo, Wenger alikuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kuwa mkurugenzi wa michezo kwenye kikosi cha PSG, lakini sasa anaweza kwenda kukamatia kazi hiyo ambayo italipa zaidi.

Wenger siku zote amekuwa na ndoto za kwenda kuwa kocha wa timu ya taifa na pengine sasa huo unaweza kuwa wakati mwafaka kwake katika kutimiza ndoto hiyo ya muda mrefu.

Umri wake wa sasa ni miaka 69, hivyo inatazamwa pia kama atakuwa na uwezo wa kunoa timu katika fainali hizo za Kombe la Dunia 2022.

Kocha Wenger alisema pia anavutiwa na usajili unaofanywa na Kocha Unai Emery, ambaye ametua huko Emirates kuchukua mikoba yake. Emery amesajili wachezaji kadhaa akiwamo kiungo Lucas Torreira anayefanya vizuri kwa sasa.

Advertisement