Wenger awaponda makinda wa Solskjaer

Muktasari:

United imekuwa na wakati mgumu tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson ambapo makocha waliofuata baada yake, David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho wameshindwa kufuata nyayo za kocha huyo Mscotland aliyestaafu kufundisha mwaka 2013.

LONDON, ENGLAND.LABDA tuseme nyani haoni kundule. Licha ya kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger kulaumiwa kwa kujaribu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England akitumia wachezaji makinda katika enzi zake, na yeye amemgeukia Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer na kudai hawezi kutwaa ubingwa na makinda.

United imeanza ovyo msimu huu ikishinda mechi moja, kutoka sare mbili na kufungwa moja na tayari Wenger anaamini United haina wachezaji waliopevuka vya kutosha kuweza kupata mafanikio msimu huu.

Ameweka wazi kikosi hiki ni tofauti na kile kizazi cha Manchester United cha mwaka 1992 maarufu kama Class of ’92 ambacho kilipandishwa kutoka kikosi cha vijana na kocha maarufu wa zamani, Sir Alex Ferguson na kupata mafanikio makubwa kwa kipindi kirefu.

Wenger anaamini wachezaji vijana wa United kama Scott McTominay, Mason Greenwood na Daniel James hawajajiandaa kuwa wachezaji wa kuanza katika klabu kubwa kama ya Manchester United na itakuwa vigumu kwao kupata mafanikio.

“Unapoona unajua kuwa ni mmoja kati ya mfano wa sehemu ambapo kuna vipaji lakini bado hawajajua kucheza kwa pamoja. Labda hawa wachezaji hawajapevuka vya kutosha kuweza kuibeba timu kama Manchester United,” alisema Wenger.

“Wanaweza kufuata nyayo za kile kina (Ryan) Giggs, (Paul) Scholes, (David) Beckham walichofanya kwa miaka mingi? Binafsi sijashawishika kabisa,” alisema kocha huyo Mfaransa ambaye aliachana na Arsenal Mei 2017.

Msimu huu Kocha wa United, Solskjaer ambaye alikuwa staa wa zamani wa klabu hiyo amepunguza wastani wa umri kwa wachezaji wake huku akiwatumia zaidi Mason Greenwood (17), Aaron Wan-Bissaka, Daniel James, Marcus Rashford (wote 21), Scott McTominay (22) na Andreas Pereira (23).

Umri wao umekuwa ukifananishwa na ule wa Class of ’92 ambapo Ferguson awalitumia mastaa kina David Beckham, Ryan Giggs, Gary Neville, Paul Scholes, Nicky Butt na Phil Neville kujenga msingi wa timu ambayo ilitamba kwa muda mrefu.

United imekuwa na wakati mgumu tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson ambapo makocha waliofuata baada yake, David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho wameshindwa kufuata nyayo za kocha huyo Mscotland aliyestaafu kufundisha mwaka 2013.

Mambo pia yanaonekana kuwa magumu kwa Solskjaer ambaye alianza vema kazi yake ya ukocha baada ya kutimuliwa kwa Jose Mourinho Desemba mwaka jana lakini kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele kikosi chake kilianza kupwaya kiasi cha kukosa nafasi za kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu huu.

United ilianza ligi kwa mbwembwe baada ya kuichapa Chelsea mabao 4-0 katika dimba la Old Trafford lakini ikaenda ugenini kucheza na Wolves na kutoka sare ya 1-1 kabla ya kurudi nyumbani Trafford na kuchapwa 2-1 na Crystal Palace halafu ikasafiri mpaka Southampton ambako ilitoka sare ya 1-1 tena.

Tayari United imeachwa nyuma kwa pointi saba na viongozi wa Ligi Kuu ya England Liverpool. Wakati ikiwa na pointi tano huku ikishika nafasi ya nane Liverpool ina pointi 12 na kama ilivyokuwa kwa msimu uliopita mashabiki wa United watalazimika kuzitazama timu mbili ambazo wana upinzani nazo mkubwa, Manchester City na Liverpool zikifukuzana katika uongozi wa ligi.

Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, United inatazamiwa kurudi uwanjani kesho kupambana na timu ngumu ya Leicester City ambayo inashika nafasi ya tatu nyuma ya Liverpool na City ikiwa na pointi nane.