Wenger anarudi, Madrid wamtaka

Muktasari:

Wenger baada ya kufundisha kwa miaka 20 katika klabu ya Arsenal aliondoka mwishoni mwa msimu uliopita na sasa amekuwa akihusishwa na kutakiwa na Manchester United na Real Madrid

MADRID, HISPANIA. ARSENE Wenger amesema yupo tayari kurudi kazini kuanzia Januari na jambo hilo limeripotiwa kuwashawishi Real Madrid ambao wanafikiria kumpa kazi huko Bernabeu.

Wenger amefunguka kuhusu ofa tamu anayotazamia kuipata kutoka kwa klabu ya Guangzhou Evergrande ya huko China, ambayo ipo tayari kumpa Mfaransa huyo mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Pauni 7.6 milioni.

Wenger amekuwa hana kazi kwa sasa tangu alipoachana na Arsenal mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kudumu kwenye timu hiyo kwa miaka 22, lakini sasa amesema anataka kurudi kazini mapema mwakani.

Wenger, 68, siku zote amekuwa akiivutia Real Madrid, ambayo kwa sasa ipo kwenye majanga makubwa chini ya kocha mpya, Julen Lopetegui. Wenger alishawahi kuwindwa na wababe hao baada ya kupata mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Arsenal.

Wenger alisema. “Naamini nitaanza tena kazi Januari Mosi. Sijui ni wapi, ila naona nimeshapumzika na sasa ni wakati wa kufanya tena kazi. Kwa ile miaka yangu 22 huko Arsenal, nimekuwa na uzoefu mkubwa sana katika mambo tofauti.”

Wenger aliwahi kufanya kazi Asia kwa mwaka mmoja wakati alipokuwa kwenye klabu ya Nagoya Grampus Eight ya Japan mwaka 1995 kabla ya kwenda kujiunga naArsenal, hivyo anaweza kurudi tena kwenye bara hilo na safari hii akienda kwenye Ligi Kuu China.

Guangzhou Evergrande, kwa sasa inanolewa na Mtaliano, Fabio Cannavaro, ambaye anamiliki kikosi ghali zaidi huko China baada ya timu yake kuwa na thamani ya Pauni 215 milioni. Wameshinda mataji saba ya Ubingwa wa China na ndicho kikosi anachochezea kwa mkopo kiungo wa Barcelona, Paulinho.