Wenger: Ozil? Kuna kitu hapa

LONDON, ENGLAND. ARSENE Wenger anaamini kuna ugomvi mkubwa zaidi baina ya Mesut Ozil na Arsenal na sio soka.

Kocha huyo gwiji wa Arsenal, Wenger ndiye aliyemsajili Ozil kwenda kukipiga kwenye kikosi hicho mwaka 2013.

Lakini, Wenger kwa sasa hayupo tena Arsenal, aliondoka Emirates tangu 2018 baada ya kuinoa timu hiyo kwa miaka 22, huku akimwaacha Ozil akiwa analipwa mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki.

Licha ya kulipwa mshahara mkubwa, Ozil hajacheza mechi yoyote msimu huu na amewekwa kando na kocha Mikel Arteta amekuwa akimweka benchi na hivi karibuni amempiga chini katika vikosi vyake vya Europa League na Ligi Kuu England.

Hata hivyo, Wenger alikiri kuwa na matatizo na Ozil kipindi alipokuwa kwenye klabu hiyo, lakini anaamini uamuzi wa kumtosa jumla Mjerumani huo si wa viwango na ubora wa uwanjani, bali unatokana na mambo mengine ya mabosi wa timu na mchezaji.

Wenger alisema: “Sijui nini kinatokea kwa kweli. Ninachoweza kusema ni kitu kimoja tu, wachezaji wabunifu wanakuwa makini na wakati mwingine wanahitaji kuhamasishwa. Kwa sababu kama unahitaji kupiga pasi zenye utata basi unahitaji kuwa mwenye kujiamini na wachezaji wa aina hiyo ni muhimu kwa sababu pasi zao ni hatari sana kwenye timu.

“Mesut Ozil ni mchezaji wa kipekee kabisa. Kinachotokea kwa sasa ni suala lake na mabosi wake, halihusiani na michezo, ndicho ninachokiamini.

“Huyu jamaa ameshinda vitu vingi. Ni bingwa wa dunia ni mwanasoka wa aina yake kabisa”

Ozil jana ametoa taarifa akisema licha ya yote anayopitia hatabadili msimamo wake wa kubaki klabuni hapo na atafanya mazoezi kwa bidii.