Wenger: Barca? Mmh hawachukui

Muktasari:

Barcelona mara ya mwisho kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa mwaka 2015, ambayo ilikuwa mara yao ya nne kufanya hivyo ndani ya miaka tisa.

NAPLES, ITALIA . ARSENE Wenger amewaondoa Barcelona kwenye orodha ya timu zinazoweza kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu akisema kwamba wababe hao wa Nou Camp hawana tena ule ubora wao kama zamani.

Miamba hiyo ya Hispania inatajwa kuwa kwenye nafasi ya nne katika orodha ya timu zinazopewa nafasi ya kubeba ubingwa huo wa Ulaya ambapo kwa sasa wapo katika hatua ya 16 na mtihani uliopo mbele yao ni kuisukuma nje Napoli.

Lakini, Wenger anaamini kwamba Barcelona hawa wa sasa hawana ule ubora ambao unawafanya washawishi kwamba watabeba ubingwa.

Alipoulizwa kama anadhani Barca hawana ubora wa kubeba taji la Ulaya msimu huu, Wenger aliambia beIN Sports : “Nakubaliana na hilo. Hii Barcelona inakuwa na takwimu sawa na Napoli. Takwimu sawa za mashuti golini, lakini takwimu sawa za kupigiwa mashuti 13 golini kwao. Naijua Barcelona ile, inakuwa na mashuti 27 kuelekea goli la mpinzani na wao wanaruhusu mashuti mawili tu.”

Barcelona mara ya mwisho kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa mwaka 2015, ambayo ilikuwa mara yao ya nne kufanya hivyo ndani ya miaka tisa.

Walishindwa kufika fainali msimu uliopita ambapo walitupwa nje na Liverpool kwenye hatua ya nusu fainali, lakini walifanikiwa kwenda kutetea ubingwa wao wa La Liga kwenye ligi ya ndani.

Wenger alipoulizwa kama kuna kitu kimebadilika kuhusu Barcelona, alisema: “Wanachelewa sana kuurudisha mpira kwenye umiliki wao, wanarudi nyuma pia kukaba.”

“Wamekuwa wazi zaidi kwenye kiungo, hawatengenezi nafasi na hawana wafungaji wa mabao kutoka kwenye kiungo ambapo Frenkie de Jong amekuwa mtu wa kukaa tu katikati, Sergio Busquets hivyo hivyo, hakuna mchezaji wa katikati anayesogelea boksi la wapinzani.”